ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka mitano tangu afariki aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa viongozi na wananchi kumuenzi na kumkumbuka hayati Dkt. Magufuli kwa mchango wake mkubwa katika kulitumikia taifa kwa bidii, uzalendo na dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
"Kesho, tarehe 17 Machi 2026, ninatarajiwa kushiriki katika Kumbukizi ya Miaka Mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Kumbukizi hiyo itafanyika Chato, Mkoa wa Geita, ambako tutapata fursa ya kumuenzi na kumkumbuka kiongozi huyu aliyelitumikia Taifa kwa juhudi na uzalendo mkubwa. Mwenyezi Mungu amrehemu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na amjaalie pepo ya milele,"ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.

