DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametangaza kuanza kwa mageuzi makubwa ya mfumo wa kodi nchini, hatua inayolenga kuujenga mfumo wa kisasa unaozingatia utoaji huduma bora, ufanisi na ukuaji wa uchumi.
Hayo yanajiri baada ya Machi 18,2026 Ikulu jijini Dar es Salaam kupokea ripoti ya Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi.Mageuzi hayo yanalenga kushughulikia changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikibainishwa na wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wadau wa maendeleo kuhusu ufanisi na usawa wa mfumo wa kodi uliopo sasa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Dkt. Samia alieleza kuwa,kuundwa kwa Tume hiyo kulilenga kufanya mapitio ya kina ya mfumo wa kodi ili kuendana na hali halisi ya uchumi wa sasa.
Alibainisha kuwa, takribani miaka 35 imepita tangu kufanyika kwa mapitio makubwa ya mwisho kupitia Tume ya Mtei, jambo linaloonyesha umuhimu wa haraka wa maboresho hayo.
Rais alisisitiza kuwa, mageuzi hayo ni nguzo muhimu katika mkakati wa muda mrefu wa maendeleo wa Taifa, hususan katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Alifafanua kuwa, utekelezaji wa dira hiyo utategemea mchango wa sekta mbalimbali, ambapo asilimia 22 itatokana na mapato ya serikali, asilimia 70 kutoka sekta binafsi, na asilimia 8 kutoka taasisi za umma.
Alisisitiza umuhimu wa kuiwezesha sekta binafsi, akisema kuwa ni lazima iundwe mazingira rafiki yatakayowezesha biashara kukua na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Aidha, Rais Samia aliipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), taasisi nyingine pamoja na wananchi kwa mchango wao katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia utii wa hiari wa kulipa kodi.
Hata hivyo, alitoa wito wa kupanua wigo wa uchumi rasmi ili kuongeza idadi ya walipa kodi na kufungua vyanzo vipya vya mapato.
Katika kusisitiza dhamira ya Serikali, Rais Samia alisema amepokea na kupitia kwa makini mapendekezo 284 yaliyotolewa na tume hiyo, na kuahidi kuwa Serikali itayatekeleza.
Aliongeza kuwa, mpango mahsusi wa utekelezaji wa muda mfupi, wa kati na mrefu utaandaliwa kwa kushirikiana na wadau muhimu.
Akizungumzia umuhimu wa mageuzi hayo, Rais alisema mabadiliko haya hayaepukiki, akitumia mfano wa nyoka anayevua ngozi yake, akisisitiza kuwa mfumo wa kodi nao unapaswa kubadilika ili kuendana na wakati.
Alieleza kuwa, mageuzi hayo yatalenga kujenga mfumo wa kodi ulio wa haki, thabiti na unaotabirika, unaoeleweka kwa walipa kodi na wasimamizi, unaochochea ukuaji wa biashara na kuongeza mapato ya ndani ya serikali. Serikali inalenga kuongeza uwiano wa kodi kwa pato la taifa (tax-to-GDP ratio) hadi kufikia asilimia 18.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, alisema Tume iliongozwa na dhamira ya kubuni mfumo wa kodi unaokidhi matarajio ya wananchi na kuendana na mabadiliko ya kiuchumi.
Alisisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa walipa kodi ili kuhakikisha kila mmoja anachangia kulingana na kipato chake kwa njia iliyo rahisi, wazi, ya haki na yenye usawa.
Aidha, alibainisha changamoto mbalimbali zilizogunduliwa, zikiwemo mzigo mkubwa wa kodi katika baadhi ya sekta, udhaifu katika mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kodi, uratibu hafifu wa taasisi, pamoja na wigo mdogo wa walipa kodi.
Alionya kuwa bila mageuzi makubwa, nchi itaendelea kutegemea walipa kodi wachache huku wakibebeshwa mzigo mkubwa.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuweka uwiano kati ya ukusanyaji wa mapato na ukuaji wa uchumi, akieleza kuwa haiwezekani kuvuna bila kupanda au kukamua bila kulisha, hivyo kuna haja ya mfumo unaochochea uwekezaji na ukuaji wa biashara.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, utekelezaji kamili wa mapendekezo unaweza kuongeza mapato ya serikali kwa shilingi trilioni 11.025 ndani ya miaka mitatu, pamoja na kufikia lengo la asilimia 18 ya uwiano wa kodi kwa pato la taifa.
Rais Samia alihitimisha kwa kutoa wito kwa Serikali, sekta binafsi na wananchi kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa mageuzi hayo, akisisitiza kuwa mafanikio yatategemea dhamira ya pamoja ya kujenga mfumo wa kodi wa kisasa, wenye ufanisi na unaolenga kutoa huduma bora.
Serikali imeeleza kuwa, utekelezaji wa mageuzi hayo utafanyika kwa awamu, ukihusisha mashauriano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa shirikishi na wenye mafanikio.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Mageuzi ya Kodi
Presidential Commission on Tax Reforms
Tax Reforms





