Tanzania na Israel zaimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo na afya

DAR-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema Israel imekuwa mshirika muhimu katika sekta mbalimbali nchini, ikiwemo kilimo, afya, ulinzi na usalama, hali inayochangia kuimarika kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesema hayo katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, wakati akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Israel nchini, Mheshimiwa Gideon Behar, mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya.

Mhe. Kombo amempongeza Balozi Behar kwa uteuzi wake na kumhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini katika kipindi chote cha utumishi wake nchini.
Aidha, ameipongeza programu ya MASHAV ya Israel inayotoa mafunzo ya vitendo kwa vijana wa Kitanzania kwenye mashamba nchini humo, na kupendekeza wataalamu wa Israel kuja kufundisha moja kwa moja katika vyuo vya kilimo nchini, ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

Amebainisha kuwa, Israel imekuwa mdau muhimu katika kuimarisha huduma za afya, hususan kupitia kambi za upasuaji wa moyo kwa watoto, ambapo zaidi ya wagonjwa 2,440, wakiwemo watoto 45 wenye matatizo ya moyo, wamefanyiwa upasuaji kupitia ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Behar amethibitisha utayari wa Israel kuendeleza na kukuza ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi na diplomasia, kwa lengo la kuleta tija kwa mataifa hayo mawili.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sayansi na teknolojia ili kuzalisha wataalamu wengi watakaonufaisha nchi zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here