Tanzania na Shirika la IFC kuimarisha ushirikiano sekta binafsi na uwekezaji

DAR-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) zimethibitisha azma ya kuendeleza ushirikiano katika kukuza sekta binafsi, uwekezaji na uchumi endelevu kwa manufaa ya pande zote mbili.
Hayo yameelezwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), na Mkurugenzi wa IFC Kanda ya Afrika Mashariki, Mary Porter Peschka, yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Kombo amepongeza mchango mkubwa wa IFC katika kuimarisha sekta ya fedha nchini, hususan kupitia usaidizi kwa benki za NMB, CRDB na NBC.
Amesema, ushirikiano huo umeongeza upatikanaji wa mikopo na mitaji, na kuwa msaada muhimu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Aidha, Serikali imetambua mchango wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) katika maendeleo ya miundombinu, ikiwemo huduma za ushauri kwa miradi ya kimkakati kama mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam.

Amesema, ushiriki wa shirika hilo katika sekta za kilimo-biashara na viwanda pia umechangia kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania.

Mhe. Kombo amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuipa kipaumbele sekta binafsi kama injini ya ukuaji wa uchumi, kwa lengo la kuendeleza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa ili kufikia malengo ya maendeleo ya taifa ifikapo mwaka 2050.
Kwa upande wake, Bi. Peschka ameipongeza Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na IFC, na kueleza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na nchi katika kukuza matumizi ya teknolojia na kuandaa wataalamu watakaoongeza tija katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, kilimo na miradi ya kimkakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here