ARUSHA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Christian Makonda (Mb) amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imelipa takribani Dola za Marekani Milioni 32 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kama sehemu ya gharama za maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.

Mhe. Makonda ameyasema hayo wakati wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo walipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kimataifa wa Arusha.
Amesema, malipo hayo yameifanya Tanzania kuwa mwenyeji halali wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika, huku serikali ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa viwanja, barabara pamoja na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo.
Aidha, Mhe. Makonda ameeleza kuwa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayohusiana na maandalizi ya AFCON, serikali tayari imelipa takribani Shilingi Bilioni 2 za fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya ujenzi wa barabara na miradi mingine ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika bila migogoro.
Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kikamilifu kuandaa AFCON 2027, mashindano yanayotarajiwa kuongeza hadhi ya nchi kimichezo na kufungua fursa zaidi za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.