Tanzania yathibitisha dhamira ya Mageuzi ya Kidemokrasia na Maadili ya Jumuiya ya Madola katika Mkutano wa CMAG

LONDON-Tanzania imethibitisha dhamira yake ya kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia na kuzingatia maadili ya Jumuiya ya Madola wakati iliposhiriki katika Mkutano wa 72 wa Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CMAG) uliofanyika London tarehe 7 Machi 2026, chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Dkt. Ian Borg, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Utalii wa Malta.
Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Prof. Palamagamba J. Kabudi (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), ambaye aliwafahamisha nchi wanachama kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 pamoja na mageuzi yanayoendelea kutekelezwa.

Katika mkutano huo, Tanzania iliwasilisha maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yakiongozwa na mfumo wa kitaifa wa Kurekebisha, Kujenga Upya na Kurejesha (Repair – Rebuild – Renew) unaolenga kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kukuza maridhiano ya kitaifa na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utawala.

Mheshimiwa Prof. Kabudi pia aliufahamisha mkutano kuhusu kazi inayofanywa na Tume Huru ya Uchunguzi inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Chande Othman, pamoja na maandalizi yanayoendelea ya kuanzisha Tume ya Katiba ya Maridhiano, itakayosaidia kuendeleza mazungumzo ya kitaifa, kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuendeleza kudumisha amani na mshikamano nchini.

Aidha, Tanzania ilieleza utayari wake wa kuwezesha ziara ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano na mifumo ya Jumuiya ya Madola, pamoja na jumuiya nyingine za kimataifa, pindi itakapokamilisha taratibu za ndani ikiwemo taarifa ya Tume ya Jaji Chande.

CMAG ilipokea kwa kuridhika ushiriki wa Tanzania na kuhimiza kuendelea kwa hatua za utekelezaji wa mageuzi yaliyoainishwa katika mkutano huo, huku ikisisitiza umuhimu wa utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria na kuzingatia Mkataba wa Jumuiya ya Madola.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mheshimiwa Prof. Palamagamba J. Kabudi alisema:

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kujitolea kikamilifu katika kuzingatia misingi na maadili ya Mkataba wa Jumuiya ya Madola. Mageuzi yanayoendelea yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kukuza maridhiano ya kitaifa na kulinda utamaduni wa muda mrefu wa nchi yetu wa amani na utulivu."

Kikosi Kazi cha Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CMAG) ni chombo kikuu cha Jumuiya ya Madola kinachohusika na kusimamia masuala ya Demokrasia na Utawala bora kulingana na misingi ya Mkataba wa Jumuiya ya Madola.

Kwa sasa kundi hili linaundwa na nchi tisa wanachama walioteuliwa na Wakuu wa Serikali za Jumuiya ya Madola, ambazo ni Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada, Malaysia, Mauritius, Samoa, Zambia na Malta, ambayo ndiyo Mwenyekiti wa CMAG.

Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola pamoja na nchi wanachama wengine katika kuendeleza mchakato wa mageuzi na maridhiano nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here