TGC inavyobadili AICC na KIA majukwaa ya Kimataifa ya utambulisho wa Vito vya Tanzania

ARUSHA-Katika enzi ambayo mataifa yanashindana kujitambulisha kupitia ubora wa rasilimali na ubunifu wao, Tanzania imepiga hatua ya kipekee na ya kimkakati.
Kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), nchi imefanikiwa kugeuza Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuwa vioo vya dunia vinavyoakisi hadhi, utajiri na ubunifu wa madini ya vito ya Tanzania.

Kupitia uanzishwaji wa maduka ya kisasa ya vito vilivyoongezwa thamani, TGC haijaweka tu sehemu za mauzo, bali imeunda majukwaa ya kimataifa ya simulizi ya Tanzania, mahali ambapo mgeni anakutana na Tanzania halisi, si kwa maneno, bali kwa ubora unaoonekana kwa macho na kuguswa.
Maduka hayo yamejengwa katika maeneo yanayopokea maelfu ya wageni wa kimataifa na kitaifa kila mwaka wakiwemo wajumbe wa mikutano ya kimataifa, watalii, wawekezaji na wasafiri wa mataifa mbalimbali.

Hapa, safari ya madini ya vito ya Tanzania inaelezewa kwa vitendo: kuanzia ardhini, kupitia elimu na teknolojia ya jemolojia, hadi kufikia vito vya kisasa vilivyobuniwa kwa viwango vinavyokubalika katika soko la dunia.

Wageni wanaowasili kupitia AICC au KIA sasa wanapata fursa ya kipekee ya kumiliki vito halisi vya Tanzania kama tanzanite na aina nyingine ya madini ya vito, si kama malighafi, bali kama bidhaa za mwisho zilizosheheni ubunifu, simulizi na utaalamu wa Mtanzania.

Akizungumza kuhusu dhamira ya mpango huo, Mratibu wa TGC, Mhandisi Ally Maganga, amesema kuwa uanzishwaji wa maduka hayo ni zaidi ya biashara; ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa wa kuitumia Sekta ya Madini kama nyenzo ya maendeleo na diplomasia ya kiuchumi.
“Haya maduka ni daraja linalomkutanisha mgeni na utambulisho wa Tanzania. Kila kito kinachouzwa kinabeba ubunifu wa Mtanzania, utaalamu wa kitaaluma, na simulizi ya rasilimali zetu. Ni namna ya Tanzania kujiwasilisha Ulimwenguni kwa vitendo,” amesema Mhandisi Maganga.

Kwa upande wa utekelezaji wa kila siku, simulizi hilo linathibitishwa na mwitikio wa wateja. Edward, mmoja wa wauzaji katika maduka ya TGC, anaeleza kuwa wageni wengi huanza kwa kuvutiwa na muonekano wa bidhaa kabla ya kuguswa zaidi na hadithi iliyo nyuma ya kila kito.

“Wageni wengi husimama kwanza kwa sababu ya mvuto wa bidhaa. Lakini furaha yao huongezeka wanapofahamu kuwa vito hivi vimetengenezwa hapa hapa Tanzania. Wengi hununua kama kumbukumbu ya safari yao, au zawadi ya kipekee yenye maana,” amesema Edward.

Wageni kutoka Ulaya, Asia, Amerika na mataifa mbalimbali ya Afrika wameeleza kuridhishwa sio tu na ubora wa vito, bali pia na maelezo ya kitaalamu yanayotolewa kuhusu chanzo, aina, thamani na upekee wa kila kito.

Uzoefu huo huongeza uaminifu, huku ukijenga taswira chanya ya Tanzania kama nchi inayojua thamani ya rasilimali zake na namna ya kuzisimulia kwa ulimwengu.

Kupitia mpango huu, TGC inaendelea kujidhihirisha kama taasisi kinara katika utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito.

Sambamba na hilo, mpango huu unachangia kukuza ajira kwa vijana waliobobea katika jemolojia, ubunifu wa vito na huduma za kitaalamu, huku ukiitangaza Tanzania kama kitovu cha vito adimu duniani.
Kwa hakika, maduka ya TGC yaliyopo AICC na KIA si sehemu za manunuzi pekee, bali ni maeneo ya simulizi ya taifa, mahali ambapo kito kinageuka kuwa hadithi, na Tanzania inajitambulisha kwa ulimwengu kwa fahari, ubunifu na thamani halisi.

Umuhimu wa Vijana wa Kitanzania katika Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito

Katika safari ya Tanzania ya kujenga tasnia imara ya madini ya vito, vijana wa Kitanzania wamebaki kuwa mhimili wa msingi na nguvu kazi ya kimkakati isiyoweza kutenganishwa na mafanikio ya uongezaji thamani.

Ushiriki wao katika ukataji, ung’arishaji, ubunifu wa vito, tathmini ya thamani na masoko unaipa sekta sura mpya ya kitaalamu na endelevu, huku ukiwapatia ajira zenye ujuzi, heshima na mustakabali wa muda mrefu.

Kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), vijana wanapata fursa za kujifunza na kubobea katika taaluma za jemolojia, ubunifu wa vito, tathmini na uthibitishaji wa ubora kwa viwango vinavyotambulika kimataifa, jambo linalowawezesha kuwa washiriki kamili wa mnyororo wa thamani wa madini ya vito badala ya kuwa watazamaji wa rasilimali zao.

Hatua hiyo inaifanya rasilimali ya madini kubadilika kutoka kuwa urithi wa kijiolojia pekee na kuwa mtaji wa maarifa na fursa za kizazi cha sasa na kijacho.

Uimarishaji wa Mafunzo na Uhaulishaji wa Teknolojia Kupitia Ushirikiano wa Kimataifa

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuimarisha ubora wa ufundishaji na mafunzo ya wataalamu wazawa kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand, hatua inayofungua ukurasa mpya wa uhaulishaji wa teknolojia na utaalamu wa kimataifa katika ukataji, ung’arishaji na utambuzi wa madini ya vito.
Ushirikiano huu unalenga kuziwezesha taasisi na wataalamu wa Kitanzania kumudu teknolojia za kisasa za uongezaji thamani, kubadilishana uzoefu, na kuinua viwango vya mafunzo hadi kufikia hadhi ya masoko ya kimataifa.

Aidha, juhudi za Serikali za kujenga jengo la kisasa la ghorofa nane jijini Arusha kwa ajili ya TGC zinaonesha dhamira ya dhati ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kitaifa na kikanda cha elimu, biashara na ubunifu wa madini ya vito, huku zikiimarisha nafasi ya vijana wa Kitanzania kuwa wahusika wakuu wa tasnia hiyo ndani na nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here