TMA yataja mafanikio ya uwekezaji katika mifumo ya hali ya hewa nchini

NA DIRAMAKINI

WAKATI Dunia ikiadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani leo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeeleza mafanikio makubwa ya uwekezaji katika mifumo ya hali ya hewa, ikibainisha kuwa, hatua hizo zimeimarisha kwa kiasi kikubwa usalama wa maisha, mali na shughuli za kiuchumi nchini.
Akitoa ujumbe rasmi wa maadhimisho hayo leo Machi 23, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt.Ladislaus Benedict Chang’a amesema, kaulimbiu ya mwaka huu, “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama,” inalenga kuhimiza matumizi sahihi ya data za hali ya hewa katika kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo endelevu.

Dkt. Chang’a ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) amesema, Tanzania imeendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa kupitia uwekezaji wa kimkakati.

Ni uwekezaji unaojumuisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa vifaa vya hali ya juu na matumizi ya teknolojia bunifu katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa.

“Serikali imefanikiwa kufunga rada tano za hali ya hewa katika maeneo ya kimkakati na inaendelea kukamilisha mtandao wa rada saba nchi nzima, hatua inayoongeza usahihi wa utabiri na utoaji wa tahadhari za mapema,” amesema Dkt.Chang’a.

Ameongeza kuwa,uwekezaji huo umeambatana na usimikaji wa vituo vya kisasa vya hali ya hewa vinavyojitegemea, vipima mvua pamoja na mifumo maalum kwa sekta za anga na kilimo, hatua inayosaidia kuboresha huduma kwa watumiaji wa sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, matumizi ya teknolojia ya kisasa ikiwemo kompyuta zenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa na mifumo ya utabiri yameongeza ufanisi katika uchambuzi wa data na utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati.

Amesema,hatua hizo zina mchango mkubwa katika kupunguza athari za majanga ya asili yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na mafuriko, ukame na dhoruba, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa ukubwa na mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, amesema TMA inaendelea kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa na kuongeza uwezo wa utoaji wa tahadhari za mapema.

Amesema, ushiriki wa wataalamu wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, ikiwemo Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), ni ishara ya mchango wa nchi katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa duniani.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna umuhimu wa kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa huduma hizo zinachangia kikamilifu katika kulinda maisha na kukuza uchumi.

“Ni muhimu kwa kila mwananchi kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa katika shughuli zake za kila siku ili kupunguza hatari na kuongeza tija,” amesisitiza.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati dunia ikiendelea kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, hali inayoongeza umuhimu wa uwekezaji katika mifumo ya hali ya hewa kama nyenzo muhimu ya ustahimilivu wa jamii.

Vile vile, Dkt.Chang’a ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana katika kuimarisha huduma za hali ya hewa, akibainisha kuwa usalama wa kesho unategemea hatua zinazochukuliwa leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here