DODOMA-Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini kimefanya uchaguzi wake wa viongozi kwa mafanikio, hatua inayolenga kuimarisha uwakilishi na kuimarisha sauti ya wafanyakazi ndani ya Wizara ya Madini.
Uchaguzi huo umefanyika leo Machi 27, 2026 katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mtumba jijini Dodoma, na kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu na misingi ya kidemokrasia, ukihusisha ushiriki mpana wa wanachama wa chama hicho.
Katika uchaguzi huo, Joseph Ngulumwa amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Madini, huku Joseph Makwinya akichaguliwa kuwa Katibu wa Tawi.
Wajumbe waliochaguliwa ni pamoja na Dorice Kagya, Deogratius Oreku na Mohamed Ngido, ambao kwa pamoja wataunda timu ya uongozi itakayohakikisha maslahi ya wafanyakazi yanawakilishwa ipasavyo.Aidha, uchaguzi huo umehusisha pia Kamati ya Wanawake ngazi ya Tawi, ambapo Felister Blandes amechaguliwa kuwa Mwenyekiti, akisaidiwa na Erieth Mgeni kama Katibu na Sarah Itambu kama Mwekahazina.
Wajumbe wa kamati hiyo ni Experansia Biseko na Selina Jama, wakitarajiwa kuwa chachu ya kuendeleza ajenda za usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake mahali pa kazi.
Akizungumza mara baada ya kusimamia zoezi hilo, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samweli Nyungwa, ameeleza kuwa uchaguzi wa vyama vya wafanyakazi una umuhimu mkubwa katika kuimarisha sauti ya wafanyakazi na kuhakikisha haki zao zinalindwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Amefafanua kuwa, jukumu la viongozi waliochaguliwa ni pamoja na kusimamia maslahi ya wanachama, kushirikiana na menejimenti katika kuboresha mazingira ya kazi, pamoja na kuhakikisha mawasiliano yenye tija kati ya wafanyakazi na waajiri yanaimarika.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uadilifu, uwajibikaji na mshikamano katika kutekeleza majukumu hayo ili kufikia malengo ya chama.
Uchaguzi huo unaashiria mwanzo mpya wa uongozi ndani ya TUGHE Tawi la Wizara ya Madini, huku matarajio yakiwa ni kuendelea kuimarisha ustawi wa wafanyakazi sambamba na kuchangia maendeleo ya sekta ya madini nchini.

















