DODOMA-Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Gallus Hyera, ametoa wito kwa askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kushirikiana kwa karibu katika juhudi za kuzuia uhalifu kabla haujatokea, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini.
Akizungumza Machi 17, 2026 katika kikao kazi kilichofanyika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Kamanda Hyera alisema kuwa kuzuia uhalifu ni jukumu la pamoja linalohitaji mshikamano kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Alibainisha kuwa, kupitia utoaji wa elimu kwa wananchi na kuimarisha mahusiano mema, inawezekana kabisa kupunguza vitendo vya kihalifu.
“Inawezekana kabisa kuzuia uhalifu kabla haujatokea kwa kuendelea kutoa elimu na kushirikiana na wananchi,” alisema Hyera, akihimiza askari kuongeza juhudi katika kuwafikia wananchi na kuwajengea uelewa juu ya mbinu za kujilinda na kutoa taarifa za uhalifu.
Aidha, aliwataka Polisi Kata kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutambua viashiria vya uhalifu na umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati, hatua ambayo itasaidia kuzuia matukio kabla hayajatokea.
Kabla ya kikao hicho Kamanda Hyera alifanya ukaguzi wa gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake pamoja na kukagua vifaa mbalimbali vinavyotumika katika utoaji wa huduma kwa wananchi wilayani humo, akisisitiza umuhimu wa askari kutunza vitendea kazi ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
