ARUSHA-Ujumbe kutoka Wizara ya Madini Makao Makuu, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Augustino Olal umetembelea Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) katika duka la kituo hicho lililopo ndani ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jijini Arusha.
Ziara hiyo imelenga kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho pamoja na kujadili mikakati ya kukuza sekta ya uongezaji thamani wa madini nchini, hususan madini ya vito ambayo Tanzania imejaliwa kuwa nayo kwa wingi.
Katika mazungumzo hayo, pande zote zimejadili umuhimu wa kuimarisha uelewa kwa wageni na wananchi wa ndani kuhusu thamani ya madini ya vito pamoja na bidhaa zinazotengenezwa kutokana na rasilimali hizo.
Aidha, imeelezwa kuwa juhudi za pamoja zinahitajika ili kuongeza ushindani wa bidhaa za madini katika soko la kimataifa.Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mratibu wa TGC, Ally Maganga, amesema kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo ni hatua muhimu katika kuinua sekta ya madini nchini.
“Tunaamini kupitia ushirikiano huu, tunaendelea kuinua ubora, thamani na hadhi ya madini ya Tanzania katika soko la kimataifa,” amesema Maganga.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uongezaji thamani na uendelezaji wa bidhaa za madini zinazozalishwa nchini.

