NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa Machi 19, 2026, ikieleza kuwa maeneo mengi nchini yanatarajiwa kuwa na hali ya mawingu pamoja na mvua, huku sehemu chache zikikumbwa na ngurumo za radi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa ya ukanda wa pwani ikiwemo Dar es Salaam, Tanga na Pwani, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, inatarajiwa kushuhudia vipindi vya mvua vitakavyokatizwa na vipindi vifupi vya jua.
Aidha, maeneo ya kaskazini na nyanda za juu yanatarajiwa kuwa na hali ya ubaridi wa kiasi, sambamba na mvua za hapa na pale.
TMA imebainisha uwepo wa uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo nchini. Mikoa iliyotajwa kuathirika ni pamoja na Kigoma, Katavi, Rukwa, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani na visiwa vya Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wanaoishi katika maeneo tajwa wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza, hususan mafuriko ya muda mfupi.
Kwa upande wa hali ya bahari, mamlaka hiyo imeeleza kuwa, mawimbi yanatarajiwa kuwa madogo, huku upepo ukivuma kutoka kusini mashariki kwa kasi ya takribani kilomita 20 kwa saa katika ukanda wote wa pwani.
Kuhusu hali ya joto, TMA imeeleza kuwa miji mbalimbali itakuwa na viwango vya wastani wa joto.
Dar es Salaam inatarajiwa kuwa na nyuzi joto kati ya 24°C hadi 30°C, Arusha kati ya 16°C hadi 26°C, huku Tanga na Zanzibar zikifikia hadi 32°C.
Kwa upande mwingine, miji ya nyanda za juu kusini ikiwemo Njombe na Mbeya inatarajiwa kuwa na hali ya ubaridi zaidi ikilinganishwa na maeneo ya pwani.
TMA imeongeza kuwa, mabadiliko madogo ya hali ya hewa yanatarajiwa kuendelea hadi siku ya Jumamosi, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa ili kuchukua tahadhari stahiki.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
