NA DIRAMAKINI
KATIKA hatua inayofungua ukurasa mpya wa historia ya safari za anga, wanaanga wanne wa ujumbe wa Artemis II wa Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA) wamefanikiwa kuingia katika eneo la mvuto mkuu wa mwezi.
Hapa ni mahali ambapo nguvu ya uvutano wa mwezi inaanza kutawala dhidi ya ile ya Dunia.
Tukio hili linachukuliwa kuwa ishara ya kurejea rasmi kwa safari za binadamu kuelekea mwezini kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 50.
Kwa mujibu wa taarifa za NASA, hatua hiyo muhimu ilifikiwa baada ya siku nne, saa sita na dakika mbili tangu kuanza kwa safari, wakati chombo chao kilipokuwa umbali wa takribani kilomita 62,800 kutoka mwezi na kilomita 373,400 kutoka Dunia.
Mafanikio haya yanaweka msingi wa hatua nyingine muhimu inayotarajiwa kufuata ambapo kuingia upande wa mbali wa mwezi, hali itakayowaweka wanaanga hao katika umbali mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu kutoka sayari ya Dunia.
Lori Glaze, mmoja wa maafisa wa NASA akizungumza kuhusu maendeleo hayo alieleza kuwa,maandalizi ya hatua inayofuata yamekamilika, huku timu za uendeshaji na wanasayansi zikiwa tayari kwa mzunguko wa kwanza wa karibu na mwezi kufanyika kwa mara ya kwanza tangu enzi za programu ya Apollo iliyokoma mwaka 1972.
Ujumbe wa Artemis II unawakilisha mabadiliko ya kimkakati katika mbinu za uchunguzi wa anga.
Aidha,tofauti na safari za Apollo ambazo zilipita karibu zaidi na uso wa mwezi, safari hii inapita katika umbali wa zaidi ya kilomita 6,400 kutoka uso huo.
Umbali huo unalenga kutoa mtazamo mpana zaidi wa jiografia ya mwezi, ikiwemo maeneo ya ncha zake ambayo yana umuhimu mkubwa katika tafiti za kisayansi na mipango ya makazi ya baadaye.
Katika kipindi cha mzunguko wa takribani saa sita, wanaanga watatekeleza uchunguzi wa moja kwa moja kwa macho pamoja na kurekodi taswira kwa kutumia vifaa maalum vya hali ya juu.
Miongoni mwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni upande wa mbali wa mwezi ambapo eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa na taarifa chache kutokana na changamoto za mawasiliano katika safari zilizopita.
Kama ilivyo kwa misheni nyingi za aina hii, mawasiliano kati ya chombo cha Orion na Dunia yatakatika kwa takribani dakika 40 wakati kitakapopita nyuma ya mwezi.
Wanaanga wanaoshiriki katika ujumbe huo ni Christina Koch, Reid Wiseman, Victor Glover na Jeremy Hansen, ambao wanatarajiwa kuweka rekodi mpya ya umbali mkubwa zaidi kuwahi kufikiwa na binadamu kutoka Dunia.
Rekodi hiyo inaashiria si tu mafanikio ya kiteknolojia, bali pia hatua ya kisaikolojia katika kupanua mipaka ya uwepo wa binadamu angani.
NASA imeeleza kuwa data itakayokusanywa katika safari hii ni nguzo muhimu kwa maandalizi ya misheni zijazo, hususan Artemis III inayolenga kutua kwa binadamu mwezini mwaka 2027, na Artemis IV inayotarajiwa kufanyika mwaka 2028.
Kwa mtazamo mpana, mafanikio ya Artemis II yanachukuliwa kuwa daraja la kuelekea malengo makubwa zaidi, ikiwemo safari za binadamu kwenda sayari ya Mirihi katika miongo ijayo.
