DCEA yakamata kilo 1,983 za dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetangaza mafanikio makubwa katika operesheni zake za mwezi Machi, 2026 baada ya kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya na kuvunja mitandao mipya ya usafirishaji wa mirungi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 13, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema kuwa, katika kipindi hicho pia zilikamatwa kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, pamoja na vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Aidha, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku jumla ya watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.

Vyombo vya usafiri vilivyotumika katika uhalifu huo ikiwemo magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja, navyo vilikamatwa.

Kwa mujibu wa DCEA, uchambuzi wa takwimu umeonesha ongezeko kubwa la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na asilimia 64 ya jumla ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo.

Amefafanua kuwa,hali hiyo inatokana na mkakati wa mamlaka kujikita zaidi katika operesheni za mashambani, kufuatia kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa kwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.

Katika Jiji la Dar es Salaam, kilogramu 101.2 za mirungi zilikamatwa katika eneo la Tegeta Kibo, zikiwa zimefichwa kwenye basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood (T 181 EMJ) lililokuwa likisafiri kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam. Dawa hizo zilifichwa katika mfumo wa hewa (AC) wa basi hilo ili kukwepa kugundulika.

Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39).

Mkoani Pwani, kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa njiani kuelekea Dar es Salaam, huku mkoani Mwanza kilogramu 52 zikikamatwa katika kizuizi cha Magu na Bandari ya Mwanza South, zikiwa zimefichwa ndani ya gari aina ya Fuso (T 296 APA) pamoja na mizigo ya mitumba. Dereva Hassan Hassan (37) alikamatwa.

Wilayani Misungwi, Mwanza, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa ndani ya nyumba na vyombo vya usafiri, zikiwahusisha Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55).

Mkoani Tanga, jumla ya kilogramu 196.96 za mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti, ikiwemo kilo 32.95 zilizofichwa kwenye mfuko pamoja na maembe. Mtuhumiwa Seif Omar (38), maarufu kama Haniwao, alikamatwa.

Katika mkoa wa Arusha, wilayani Longido, kilogramu 106.25 za mirungi zilikamatwa zikiwa kwenye gari aina ya Toyota Wish (T 889 DPG), ambapo watuhumiwa wawili akiwemo diwani walitiwa mbaroni. Aidha, kilo 138.42 zilikamatwa katika matukio mengine ya mkoani humo.

Kwa upande wa Kilimanjaro, maeneo ya Himo na Same, kilogramu 68.3 za mirungi zilikamatwa na watuhumiwa wawili kutiwa nguvuni.

Mbali na mirungi, DCEA ilikamata paketi 141 za bangi aina ya skanka katika hosteli ya wanafunzi iliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mtuhumiwa Semvua Sangi (31), msimamizi wa hosteli hiyo, alikamatwa baada ya dawa hizo kupatikana chumbani kwake.

Mamlaka imeonya kuwa tukio hilo linaashiria uwepo wa biashara ya dawa za kulevya karibu na taasisi za elimu, na kutoa wito kwa jamii kushirikiana kudhibiti hali hiyo.

Katika Mkoa wa Songwe, eneo la Tunduma, kilogramu 8.2 za bangi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Mbeya. Kwa ujumla, kilogramu 707.995 za bangi zilikamatwa katika operesheni mbalimbali nchini.

Katika jitihada za kudhibiti kemikali bashirifu, DCEA kwa kushirikiana na taasisi nyingine ilifanya ukaguzi katika kampuni, maduka ya dawa, na bandari kavu. Ukaguzi huo uliwezesha kuzuiliwa kwa kemikali hatarishi ikiwemo potassium permanganate, hydrochloric acid, acetone, sulphuric acid na acetic acid glacial.

Vilevile, dawa tiba zenye asili ya kulevya kama alprazolam, midazolam, clonazepam, fentanyl, zolpidem, tramadol, codeine na dihydrocodeine zilikamatwa.

Amesema, dawa hizo kitaalamu, huweza kusababisha uraibu iwapo zitatumika bila udhibiti.

Kwa ujumla, operesheni za mwezi Machi zimeakisi dhamira ya Serikali ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya nchini. Hata hivyo, DCEA imebaini kuwepo kwa mitandao mipya ya usafirishaji wa mirungi pamoja na mbinu mpya za kuficha dawa hizo.

Mamlaka imeeleza kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za udhibiti na wananchi ili kuziba mianya yote ya uhalifu huo, huku ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila kujali hadhi yake katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here