Basi la Abood lakamatwa likiwa na dawa za kulevya, zilifichwa kwenye mfumo wa hewa

NA DIRAMAKINI

BASI la abiria aina ya Yutong linalomilikiwa na kampuni ya Abood, lenye namba ya usajili T 181 EMJ, limekamatwa likiwa limebeba kilogramu 101.2 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika eneo la Tegeta Kibo jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 13,2026 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Ukamataji huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, ni matokeo ya operesheni kabambe iliyoendeshwa na DCEA katika kipindi cha mwezi Machi, 2026,

Amesema kuwa,basi hilo lilikuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania ambapo dawa hizo zilikuwa zimefichwa kwa ustadi mkubwa katika maeneo mbalimbali ya chombo hicho cha usafiri, ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC), kwa lengo la kukwepa kugundulika.

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi hilo, Ramadhan Mohamed (52), kondakta Salma Sanga (26), pamoja na Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39), ambao kwa sasa wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Katika operesheni nyingine mkoani Pwani, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, jumla ya kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea jijini Dar es Salaam, hali inayoashiria kuwepo kwa mtandao mpana wa usambazaji wa dawa hizo.

Aidha, mkoani Mwanza, jumla ya kilogramu 52 za mirungi zilikamatwa katika kizuizi cha barabarani cha Magu na Bandari ya Mwanza South.

Dawa hizo zilikuwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Fuso lenye namba ya usajili T 296 APA, zikiwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba.

Amesema,dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina, Nyamagana, alikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Katika tukio lingine wilayani Misungwi mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa ndani ya nyumba na katika vyombo mbalimbali vya usafiri.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55). Vyombo vilivyotumika katika usafirishaji ni pamoja na magari aina ya Toyota Crown (T 742 EGL), Toyota Wish (T 854 DXB) na bajaji yenye namba MC 261 EZV.

Mkoani Tanga, kiasi cha kilogramu 32.95 za mirungi kilikamatwa kikiwa kimefichwa ndani ya mfuko na kuchanganywa na maembe ili kuficha uhalisia wake.

Katika tukio hilo, Seif Omar (38) maarufu kama “Haniwao”, mkazi wa Mtaa wa Taifa, Barabara ya 13 na mjumbe wa Serikali ya Mtaa, alikamatwa.

Vilevile, operesheni nyingine mkoani humo zilisababisha kukamatwa kwa jumla ya kilogramu 164.01 za mirungi katika matukio tofauti.

Kwa upande wa Mkoa wa Arusha, wilayani Longido, kilogramu 106.25 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish lenye namba ya usajili T 889 DPG.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Solomon Koholo (38), Diwani wa Kata ya Kimokouwa, pamoja na Lekaneti Kukuu (38). Aidha, katika matukio mengine mkoani humo, kilogramu 138.42 za mirungi zilikamatwa.

Kadhalika, mkoani Kilimanjaro katika maeneo ya Himo na Same, jumla ya kilogramu 68.3 za mirungi zilikamatwa, zikiwahusisha watuhumiwa Amin Mazua (58), maarufu kama “Mbaruku”, na Wilbard Mchau (50).

Kamishna Jenerali Lyimo amesisitiza kuwa, sambamba na operesheni za kudhibiti mirungi, mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha doria na uchunguzi dhidi ya aina nyingine za dawa za kulevya nchini.

Pia ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti na hatimaye kutokomeza biashara ya dawa za kulevya nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here