DAR-Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Dkt.Fred Msemwa leo amefungua Baraza la Kwanza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi(TISEZA), baada ya kuundwa kwake kwa kuunganisha TIC na EPZA.
Akifungua kikao hicho, Dkt. Msemwa aliwataka watumishi wa TISEZA kuondoa hulka ya kufanya kazi kwa mazoeea kutokana na mchango mkubwa walionao katika kuchangia Pato la Taifa.
Alisema DIRA 2050 imeelekeza asilimia 70 ya Pato la Taifa lichangiwe na Sekta Binafsi ambapo uwekezaji upo ndani yake.
"Katika hilo, TISEZA mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha Tanzania inakuwa kimbilio la uwekezaji wa ndani nje; na ninyi kama Baraza la Wafanyakazi mna mchango mkubwa wakuufanya TISEZA ifanikiwe," alisema.
Aliwakata Wafanyakazi wa TISEZA kuwa wakarimu wa wawekezaji ili waione Tanzania ni mahali sahihi pa uwekezaji.

Awali, akimkaribisha, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Terry alisema katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2026 miradi 177 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.2 imesajiliwa huku ikitoa ajira 19,750.
Bw. Terry alishukuru kwa ushirikiano anaoupata kutoka Ofisi ya Rais, Uwekezaji ambao unakuwa ni chachu ya kufanya maendeleo endelevu katika uwekezaji.
Akisema katika kutoa kipaumbele kwenye mradi wa Bagamoyo, TISEZA imeamua kuuundia kurugenzi maalumu kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unakuwa na tija.
