BAHI-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI),Mhe.Prof. Riziki Shemdoe, amesema iwapo atapewa taarifa ya uhakika ya afisa yeyote anayepaswa kuwahudumia walimu na kutatua kero zao, kwamba amemuonea au kutomtendea haki mwalimu yeyote hatosita kumuondoa katika cheo alichonacho.
Prof. Shemdoe ametoa tahadhari hiyo Aprili 17, 2026 akiwa wilayani Bahi, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa darasa la nne, saba, kidato cha pili na cha nne wa wilaya ya Bahi, iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Chiona wilayani humo.
“Tutatue kero za walimu kwa wakati, nitakuwa mkali na sitomfumbia macho afisa yeyote wa idara ya elimu atakayemuonea au kutomtendea haki mwalimu, nitachua hatua ya kumuondolea cheo alichonacho kwani atakuwa ameugusa moyo wangu,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameanisha kuwa, kuna maeneo yana changamoto ya kuwahudumia walimu akitoa mfano wa mahali alipokwenda kukagua utendaji kazi na kukuta mwalimu amesafiri umbali wa kilomita 200 kufuata huduma ambayo anapaswa kupatiwa kwa muda usiozidi dakika 10, lakini mwalimu anaambiwa aje siku inayofuta, hivyo kumuongezea gharama na usumbufu unaoepukika.
Prof. Shemdoe amehimiza kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kupeleka tabasamu kwa walimu, kwa wazazi na wanafunzi ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi na ndio maana hatosita kumchulia hatua afisa yeyote atakayebainika kumuonea au kutomtendea haki mwalimu ambaye amepewa jukumu la kuhakiksha mwanafunzi anapata ufaulu mzuri.






