Waziri wa Fedha, Balozi Omar aishauri Benki ya Dunia kuiwezesha sekta binafsi

NA BENNY MWAIPAJA,
WF-Washington D.C

WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ameishauri Benki ya Dunia kuangalia namna ya kuiwezesha sekta binafsi katika nchi za Afrika ili iweze kuwa imara na kuchangia kukuza uchumi wa nchi hizo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakifuatilia mada mbalimbali katika Mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency) wanachama wa Benki ya Dunia, uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo, jijini Washington D.C nchini Marekani, wakati wa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WF, Washington D.C. Marekani).

Mhe. Balozi Omar, ametoa wito huo wakati akichangia mada katika mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika, wanachama wa Benki ya Dunia (Africa Group 1 Constituency), uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Amesema kuwa, wakati nchi za Afrika zinatakiwa kuongeza ufanisi katika kukusanya mapato yake ya ndani, sekta binafsi za nchi wanachama wa Benki ya Dunia ikiwezeshwa kikamilifu, inaweza kuvutia mitaji ya ndani sawa na mitaji ya nje.

Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na madeni yanayofikia ukomo wa kuendelea kukopa zaidi, hivyo njia ya kujikwamua na changamoto hiyo ni kuongeza makusanyo ya mapato yao ya ndani kwa kutoza kodi kubwa ambazo kwa namna moja au nyingine zinaathiri kundi kubwa la wananchi masikini.

Alishauri Benki ya Dunia kutumia mbinu za Mpango wa Marshall (Marshall Plan) kuzisaidia nchi za Afrika, mpango ulioanzishwa na Marekani mwaka 1947 ili kuziwezesha nchi za ulaya kukabiliana na athari za vita ya pili ya dunia, hatua iliyosaidia nchi hizo kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa, kupata usaidizi wa teknolojia, kukuza biashara na kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza katika Mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency) wanachama wa Benki ya Dunia, uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo, jijini Washington D.C nchini Marekani, wakati wa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.

Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Dunia kwa Kundi la kwanza la Kanda ya Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dkt. Zarau Wendelin Kibwe, alisema kuwa Benki ya Dunia inatarajia kukusanya na kutumia dola za Marekani bilioni 100 kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na changamoto za kiuchumi pamoja na kukuza sekta binafsi.

Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ujumuishaji kwa kupanua fursa za ajira kwa wanawake, vijana, na jamii zisizopewa kipaumbele huku ikiimarisha ulinzi wa kijamii na ustahimilivu kutokana na mabadiliko ya kiuchumi.

Aidha, Dkt. Kibwe alisema kuwa juhudi hizo kwa pamoja hazilengi tu kuunda ajira, bali pia kuhakikisha ajira hizo ni za uzalishaji, endelevu, na zinapatikana kwa wote kupitia Ajenda ya Ajira katika kubuni miradi (Agri-Connect, Nishati, Afya, na Madini) na kuweka kipaumbele kwenye sekta zinazozaa ajira kwa lengo la kuunda fursa zaidi za ajira kwa vijana.

Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika wanachama wa Benki ya Dunia (Africa Group 1 Constituency) limeundwa na nchi 22 kutoka Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania, Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here