Hii gesi asilia

NA LWAGA MWAMBANDE

HALI ya sasa ya soko la mafuta duniani imesababisha changamoto kubwa kiuchumi kwa nchi zinazotegemea nishati ya nje, hivyo mataifa mengi yanaangalia mbadala wa nishati hususani gesi asilia.
Tanzania, nchi iliyo tajiri kwa rasilimali za gesi asilia ikiwa na akiba inayokadiriwa kufikia futi trilioni 57.54, ina nafasi ya kipekee ya kutumia akiba yake ya gesi kujinasua na kupunguza athari za bei za mafuta zinazopanda kimataifa.

Gesi inaweza kubadilishwa kuwa kimiminika (LPG), umeme na mafuta kwa ajili ya kuendeshea magari au viwanda,hivyo kupunguza utegemezi wa petroli na dizeli za nje.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, kuanzisha akiba ya taifa ya gesi na kuboresha miundombinu ya usambazaji kutasaidia kuongeza usalama wa nishati na kupunguza gharama kwa wananchi.

Pia,Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kutumia rasilimali zake kwa maendeleo endelevu na kushinda changamoto za mfumuko wa bei za mafuta. Endelea;

1. Sasa gesi asilia, iliyopo Tanzania,
Ni vema tukatumia, makali jipunguzia,
Hali hii ya dunia, ambayo tunapitia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

2. Vile watutangazia, hapa zilipofikia,
Hatuwezi kujulia, kesho zitapoishia,
Hii gesi asilia, ni yetu twajichimbia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

3. Wale walitangulia, mitungi kuichimbia,
Kwenye magari sikia, bei wanafurahia,
Ila waliobakia, bei hizi wanalia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

4. Gesi hii asilia, wengi sasa watumia,
Tena wanafurahia, makali wapunguzia,
Hata mazingira pia, vema inasaidia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

5. Shida iliyosalia, hii gesi asilia,
Vituo kutupatia, kotekote kufikia,
Dasalamu nakwambia, kwa wilaya zote pia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

6. Na kidogodogo pia, mikoani kuingia,
Kwanza Pwani kufikia, Moro na Dodoma pia,
Hii kweli nakwambia, wengi itasaidia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

7. Huko Lindi na Mtwara, ambako twajichimbia,
Gesi asilia bora, wao kuwasambazia,
Hii bei ya hasara, hawawezi kuingia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

8. Yatufundisha dunia, haya yanatufikia,
Bila ya kuangalia, uwezo utafifia,
Fedha nyingi kitumia, mafuta kuagizia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zitatunyonga.

9. Gesi asilia jibu, linaweza saidia,
Kutumia taratibu, sote kutatuingia,
Kisha tuwe na sababu, maisha kufurahia,
Hizi bei za mafuta, kwa kweli zinatunyonga.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here