NA LWAGA MWAMBANDE
MGOGORO kati ya Marekani, Israel na Iran umeibua taharuki kubwa katika masoko ya kimataifa, hasa kwa kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta, kuvuruga mnyororo wa usambazaji na kuathiri uwekezaji wa kimataifa.
Picha na Mtandao.
Ni wazi kuwa, mataifa ya Afrika yanayotegemea mafuta ya nje kwa sasa yanakabiliwa na gharama kubwa za nishati, mfumuko wa bei na changamoto za chakula.
Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) limeonya kwamba mizozo hii inaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa dunia, kukuza gharama za maisha na kuathiri mataifa yanayoingiza mafuta mengi.
Mataifa yasiyo na uzalishaji mkubwa wa nishati, ambayo ni pamoja na mengi ya Afrika, yanadumaza ukuaji wa uchumi kutokana na gharama ya juu ya mafuta na mbolea.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Afrika inazalisha mafuta kidogo ukilinganisha na mahitaji yake, hivyo inategemea usafirishaji wa ghuba na mafuta ya nje, na kusababisha gharama ya kusafirisha bidhaa kupanda.
Pia, kupanda kwa bei ya mafuta kuna athari mbaya kwenye uzalishaji wa mbolea na chakula, hivyo kusababisha gharama za kilimo na usalama wa chakula kushuka.
Mzozo huu pia unaweza kupunguza mtiririko wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka mataifa tajiri, jambo ambalo Afrika inategemea kwa miradi ya maendeleo.
Kutokana na changamoto hii, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anashauri mataifa ya Afrika kuboresha ushirikiano wa kikanda, kujenga akiba ya nishati, kukuza uzalishaji wa ndani wa nishati mbadala na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ili kupunguza athari za mzozo huu wa kimataifa.Endelea;
1. Ni jiwe la utosini, watupiga Marekani,
Kwa wewe kwenda vitani, ukimpiga Irani,
Twateseka duniani, kosa letu hatuoni,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
2. Mabomu yanarindima, watu wenda mautini,
Watu walisemasema, ni mateso duniani,
Tulidhani huko noma, ishatufika nyumbani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
3. Hilo la moja kwa moja, limetukaba kooni,
Mafuta kwa lita moja, tunachimba mfukoni,
Zaidi ya elfu moja, bei mepaa hewani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
4. Wawili tamaa zao, kumdhibiti Irani,
Madhara si peke kwao, ambao wako vitani,
Hata majirani zao, nasi tuloko pembeni,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
5. Ongezeko elfu moja, ni kuwa sana jamani,
Hapa ninajenga hoja, vipato vyaenda chini,
Na hatua moja moja, tutatembea njiani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
6. Hasa kwa wafanyakazi, ndio wakabwa shingoni,
Mshahara kama kazi, haupanda asilani,
Yanapaa matumizi, wao wainama chini,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
7. Kwa wafanyabiashara, shari kama hawaoni,
Bei tazifanya bora, kwani wanajali nini,
Hawaangalii sura, hasara kwao ya nini?
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
8. Haya yanapotea, iingie akilini,
Tusijekuendelea, tukaishi kizamani,
Pesa tukazichezea, zikaishia njiani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
9. Muda kufunga mkanda, kutilia maanani,
Kote kule tunakwenda, tufanye yenye thamani,
Gharama zisijepanda, tuingie msambweni,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
10. Chonde chonde Marekani, watupeleka shimoni,
Acha ipiga Irani, nasi tuwe na amani,
Mafuta bei za ndani, kwetu ziwe ahueni,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
11. Suluhisho la kudumu, nyote kukaa mezani,
Sheria kuziheshimu, zilizopo duniani,
Ili amani idumu, tusiingie shidani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
12. Mkizidi kuzipiga, shida kubwa duniani,
Hizi zote zetu swaga, zitaishia shimoni,
Utabaki wenu uga, sisi tukiwa shidani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
13. Mwatupiga utosini, mwili hauna amani,
Sisi nyasi ziko chini, twaumia hadi ndani,
Jamani angalieni, twateseka duniani,
Wakizipiga wababe, ziumiazo ni nyasi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
