Hospitali ya Jiji Dodoma yaipongeza MSD kwa usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati

NA GODFREY NNKO

HOSPITALI ya Jiji la Dodoma imeipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati, hali inayochangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa leo Aprili 23, 2026 na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joshua Mwalongo, wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea hospitali zinazohudumiwa na MSD katika mikoa ya Dodoma na Singida.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Mwalongo amesema, MSD imekuwa mdau muhimu katika sekta ya afya, akibainisha kuwa vifaa vingi vinavyotumika hospitalini hapo vinatokana na bohari hiyo.

“Kwa hakika tunawashukuru sana MSD.Ni mdau mkubwa katika eneo la afya, na karibu vifaa vyote tulivyoviona hospitalini ni matokeo ya ushirikiano wao. Wamekuwa wakituunga mkono kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joshua Mwalongo.
Ameongeza kuwa,upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka MSD umekuwa wa uhakika, huku akisisitiza kuwa hata katika hali za dharura, bohari hiyo imekuwa ikijibu kwa haraka mahitaji ya hospitali.

“Dawa zinapatikana kwa wakati. Hata pale panapotokea upungufu, tunapotuma oda ya dharura, hushughulikiwa mara moja. Hii imeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” ameeleza.

Dkt. Mwalongo pia ameeleza kuwa, Hospitali ya Jiji Dodoma ilijengwa mwaka 2023 na kuanza rasmi kutoa huduma Januari 2025, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu ya afya nchini.
Katika hatua nyingine, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya afya, akibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimetumika katika ujenzi wa hospitali hiyo.

“Hospitali hii ni mpya na bado tunaendelea na ujenzi. Tayari zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimetumika katika ujenzi wake,” amesema.

Amefafanua kuwa,hospitali hiyo ina jumla ya majengo 10, huku Serikali ikitoa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vilivyopatikana kupitia MSD.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuboresha miundombinu ya barabara inayoelekea hospitalini hapo, ambapo kwa sasa kuna barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.5, tofauti na hali ya awali ambapo eneo hilo lilikuwa pori.
Kwa upande wa huduma, Dkt. Mwalongo amesema,hospitali hiyo kwa sasa inatoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, kliniki za mama, baba na mtoto, huduma za uzazi, maabara, mionzi, meno, ustawi wa jamii pamoja na huduma za kuhifadhi maiti.

Amebainisha kuwa, mwitikio wa wananchi kutumia huduma za hospitali hiyo umeongezeka kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa sasa wanahudumia wagonjwa kati ya 600 hadi 700 kwa mwezi katika huduma za nje.

Vilevile, amesema idadi ya wajawazito wanaojifungua hospitalini hapo imeongezeka kutoka mmoja kwa mwezi wakati wa mwanzo wa huduma hadi kufikia kati ya 60 na 70 kwa mwezi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwalongo, hospitali hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakitegemea huduma kutoka Hospitali ya General na Kituo cha Afya Makole, ambavyo vilikuwa vikikabiliwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa.

Amesema,Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya kwa kuongeza upatikanaji wa huduma katika hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na mpango wa kusogeza huduma zinazopatikana katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa hospitali hiyo ina watumishi wa kutosha wanaotoa huduma saa 24, akitoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kutoa ajira, hususan kwa vijana.

Aidha, amewahimiza vijana nchini kujituma na kutumia fursa za ajira zinazotolewa na Serikali ili kushiriki katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Kwa ujumla, maendeleo ya Hospitali ya Jiji Dodoma yanaakisi jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here