Safari ya kuijenga upya Tanzania yaanza baada ya uwasilishaji wa ripoti ya Tume ya Uchunguzi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Aprili 23,2026 amepokea rasmi Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Tukio hili linaashiria mwanzo wa hatua ya utekelezaji wa mapendekezo ya kuponya Taifa, kuimarisha uwajibikaji na kujenga mustakabali imara zaidi.

Akizungumza wakati wa kupokea ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais ametambua kwa uzito mkubwa madhara yaliyolikumba Taifa, akipokea maelezo kuwa matukio hayo yalisababisha vifo vya takribani watu 518, majeruhi zaidi ya 2,390, na uharibifu wa mali unaokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 125.
Amesisitiza kuwa, hasara hizi zimeacha majeraha makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisaikolojia kwa wananchi.“Hili ni janga na doa kubwa kwa Taifa letu,” amesema Rais Dkt.Samia.

Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa,kazi ya Tume imeiwezesha nchi kupata uelewa sahihi wa kilichotokea, ikijumuisha uchambuzi wa kina uliotokana na ushahidi wa mashahidi 1,323, maelezo ya viapo 953, pamoja na maoni yaliyokusanywa kupitia njia mbalimbali ikiwemo zaidi ya ujumbe mfupi 33,000 na maoni ya maelfu ya wananchi katika maeneo 202 yaliyofanyiwa uchunguzi.

“Wakati mwingine dawa ni chungu, lakini kama tunataka kupona, lazima tunywe dawa. Tume imechunguza kilichotusibu. Kazi yetu sasa ni kutumia dawa hiyo ipasavyo,” amesema Rais Dkt. Samia na kusisitiza kuwa Taifa lina wajibu wa kuhakikisha matukio hayo hayajirudii kwa kuchukua hatua za marekebisho na uwajibikaji.
Aidha, Mheshimiwa Rais amehimiza mshikamano wa kitaifa akibainisha kuwa mustakabali wa nchi uko mikononi mwa Watanzania wenyewe.

“Hatma ya Tanzania ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe.” Katika juhudi za kuliponya Taifa, ametoa wito mahsusi kwa viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maridhiano na kurejesha maadili ya jamii. “Simamieni nafasi yenu ya kuliponya Taifa letu.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, amesema kuwa,ripoti hiyo ni matokeo ya uchunguzi mpana uliodumu kwa siku 153, ukihusisha mikoa 11, wilaya 21, na maeneo 202 yaliyoathirika zaidi.

Ameeleza kuwa,mchakato huo ulihusisha pia mijadala ya vikundi zaidi ya 200 na ushirikishwaji mpana wa wananchi.
“Ripoti tunayoiwasilisha inabeba dhamira ya pamoja ya Taifa ya kutibu majeraha, kuwajibika kila panapostahili, lakini muhimu zaidi kujifunza na kusonga mbele,” amesema Mwenyekiti wa Tume na kuongeza kuwa, licha ya maumivu makubwa yaliyosikika kutoka kwa waathirika, Watanzania wengi walionesha utayari wa kushiriki katika safari ya maridhiano na kujenga upya mshikamano wa kitaifa.

“Waliowasiliana na Tume walionesha wazi kuwa yaliyotokea siyo taswira halisi ya Utanzania wetu.” Mheshimiwa Rais amekiri uzito wa jukumu lililopo mbele yake na kuahidi kulibeba kwa ujasiri huku akihimiza ushirikiano wa wote.

“Nataka niwahakikishie nitaubeba mzigo huu kwa ujasiri na kujiamini na hadhari kubwa. Kwa pamoja tutafanya. Tusimuachie Samia peke yake.”

Katika hatua nyingine,Mheshimiwa Rais amewataka Watanzania kujifunza kutokana na yaliyotokea na kusonga mbele kwa umoja na dhamira mpya ya kulijenga Taifa. “Tumegusa kaa la moto, na tumejifunza,” alisema.
Hii ni Tume ya saba ya Rais ya Uchunguzi tangu Uhuru. Tume iliundwa tarehe 18 Novemba, 2025 na kuanza kazi tarehe 20 Novemba, 2025. Tume ilikuwa na wajumbe tisa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Wajumbe wengine ni pamoja na Prof. Ibrahim Hamis Juma, Balozi Ombeni Yohana Sefue, Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Bw. Said Ally Mwema, Balozi George Kahema Madafa, Balozi Paul Meela, Balozi Radhia Naima Msuya na Balozi David Joseph Kapya.

Tume ilikusanya ushahidi kutoka kwa maelfu ya wananchi kupitia mbinu mbalimbali za kisayansi na kijamii ili kubaini ukweli wa matukio na kutoa mapendekezo ya kuimarisha amani, uwajibikaji na mshikamano wa kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here