Hungary kuongeza nguvu mradi wa maji Biharamulo

DODOMA-Serikali ya Tanzania na Hungary zimesaini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 55.1 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Biharamulo mkoani Kagera.
Mkataba huo umesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania akishuhudiwa na Balozi Mteule wa Hungary nchini, Mhe. Katalin Nyirati.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo Dkt. Mwamba alisema kuwa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo awali ulisainiwa na Katibu wa Nchi anayeshughulikia uhusiano ya Pande Mbili katika Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Bi. Boglárka Illés na ilibaki upande wa Tanzania kutekeleza zoezi hilo.
Dkt. Mwamba alisema kuwa hatua ya kutiwa saini kwa upande wa Tanzania, inawezesha nchi kupata mkopo huo kupitia Benki ya Exim ya Hungary kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

“Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, sambamba na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26), Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na Dira mpya ya Maendeleo ya Tanzania 2050,” alisema Dkt. Mwamba.

Alisema kuwa, pamoja na kuthamini mikopo nafuu, kuna umuhimu wa kupanua wigo wa ushirikiano ili kujumuisha pia misaada ya ruzuku katika maeneo kama vile ujenzi wa uwezo, elimu na sekta nyingine za kijamii, ili kuongeza manufaa jumuishi na endelevu kwa wananchi.
Alisisitiza dhamira thabiti ya Serikali ya kuendelea kuimarisha na kupanua ushirikiano wa pande mbili na Hungary chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kukuza ustawi wa wananchi wa nchi zote mbili.

Aidha Dkt. Mwamba alimpongeza Mhe. Balozi Nyirati kwa kuteuliwa kwake, akibainisha kuwa uteuzi huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Hungary ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kihistoria na Tanzania pia alimhakikishia Balozi huyo ushirikiano kamili kutoka Serikali ya Tanzania katika kuendeleza uhusiano wa pande mbili.

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Hungary nchini, Mhe. Katalin Nyirati, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Hungary umedumu kwa zaidi ya miaka 60 kwa kuwa Tanzania ni mshirika wa kuaminika.

Aliihakikishia Tanzania kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yenye manufaa kwa pande zote mbili ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya maji, elimu, kilimo, kisiasa na masuala ya teknolojia ambapo wako tayari kubadilishana ujuzi katika kuongeza ufanisi wa sekta hizo.

Alisema kuwa Dunia inapitia katika changamoto mbalimbali za kiuchumi hivyo ushirikiano wa dhati kati ya nchi hizo mbili utasaidia kuzihakikishia uimara wa kiuchumi na mambo mengine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, aliishukuru Hungary kwa hatua iliyofikiwa ya utoaji wa mkopo wa mradi wa Maji Biharamulo, kwa kuwa wananchi wa eneo hilo wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa mradi huo.

Alisema kuwa wananchi watafurahi kuona mkataba umesainiwa kwa kuwa unaleta matumaini mapya ya utekelezaji wa mradi huo wenye umuhimu mkubwa katika maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here