MWANZA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendesha kampeni yake ya ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’ katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza ambayo itafanyika kwa kipindi cha wiki tatu.
Kampeni hiyo iliyoanza tarehe 01 Aprili 2026, imejikita katika kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu ukopaji salama na wenye tija unaozingatia kutumia wakopeshaji wenye leseni kutoka BoT, kupitia masharti na vigezo vya mkopo, uwezo wa kurejesha, madhara ya kuchelewa au kushindwa kulipa mkopo pamoja na kukopa kwa malengo ya maendeleo.
Akizungumza wakati uzinduzi wa kampeni hiyo, Meneja wa Uchumi Tawi la BoT Mwanza, Bw. Issa Pagali, alieleza kuwa ujumbe wa kampeni hiyo unaeleweka kirahisi na una nguvu endapo wananchi watauzingatia.“Zinduka ikimaanisha kutambua haki zako na kupata elimu sahihi ya fedha, Usiumizwe ikimaanisha kuepuka mikopo yenye masharti magumu na yasiyoeleweka na Kopa kwa Maendeleo ikiwa na maana ya kutumia mikopo kama chombo cha kuboresha maisha.”, alieleza Meneja huyo.
“Nawahimiza wanamwanza, mjitokeze kwa wingi katika kampeni hii inayoendelea hadi tarehe 21 Aprili, 2026,”aliongeza.
Katika hatua nyingine, aliwataka watoa huduma za kifedha kufuata miongozo inayoambatana na leseni zao ili kuepusha uwepo wa mikopo inayowaumiza wananchi.
Miongoni mwa maeneo ambayo tayari yamefikiwa na elimu hii ni pamoja na Buseru, Pasiansi, Nyakato National na Nyamongolo Center, yote yaliyopo katika Wilaya ya Ilemela. Kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea siku ya Jumatatu, tarehe 6 Aprili, katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nyamagana.
Kampeni hii ni muendelezo wa jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na Benki Kuu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu ukopaji salama na wenye tija. Hii si mara ya kwanza kwa BoT kuendesha kampeni ya aina hii, mara ya mwisho ilifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 30 Januari hadi 28 Februari 2025.







