Kituo cha Polisi Lupaso chazinduliwa kuimarisha usalama Masasi

MTWARA-Kituo cha Polisi Lupaso kilichopo katika Kata ya Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, kimezinduliwa rasmi na Katibu Tarafa ya Chiungutwa, Mheshimiwa Ally Mohamed Kuchele, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Kuchele alieleza kuwa uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi wa eneo hilo.

Alitoa shukrani kwa Mheshimiwa  Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuridhia kutolewa kwa fedha za ujenzi wa kituo hicho.
Aidha, aliishukuru familia ya Hayati Benjamin Mkapa kwa kutoa eneo lililotumika kujenga kituo hicho.

Alifafanua kuwa kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wananchi wa kata tano pamoja na vijiji zaidi ya ishirini, hivyo kuwa chachu ya kuimarisha usalama na ustawi wa jamii katika ukanda huo.

Mheshimiwa Kuchele pia aliipongeza kamati ya ujenzi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa ubora wa jengo unaendana na thamani ya fedha zilizotumika. Alisisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kulitunza jengo hilo ili liendelee kutoa huduma bora kwa muda mrefu.
Zaidi ya hayo, alihimiza Jeshi la Polisi kutumia kituo hicho kama nyenzo ya kuzuia uhalifu kabla haujatokea, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya uhamasishaji, hususan kuhusu tahadhari za kuwapokea na kuwatambua wageni katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Issa Suleiman, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa kituo hicho.

Pia aliwashukuru viongozi wa eneo hilo, akiwemo Diwani wa Kata ya Lupaso, pamoja na kamati ya ujenzi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo.
Ujenzi wa Kituo cha Polisi Lupaso ulianza Septemba 2024 na kukamilika Februari 2026, ukiigharimu Serikali jumla ya shilingi 140,400,264.

Mradi huo unatarajiwa kuwa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama, utulivu na maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Masasi na maeneo jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here