NA DIRAMAKINI
UTEKELEZAJI wa programu ya kliniki za kisheria bila malipo kwa wananchi, sambamba na uzinduzi wa kamati za ushauri wa kisheria katika ngazi za mikoa na wilaya, umeanza kuzaa matunda kwa kurejesha haki na matumaini kwa wananchi mbalimbali nchini.
Miongoni mwa wanufaika wa huduma hiyo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Sema Limited, Bw. Ivo Manyako ambaye amerejeshewa magari yake matano yaliyokuwa yameshikiliwa kinyume cha sheria.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya magari hayo iliyofanyika leo Aprili 22, 2026 mkoani Singida, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza Johari amesema, tukio hilo ni matokeo ya kliniki ya msaada wa kisheria iliyofanyika mkoani humo kuanzia Mei 19 hadi 25,2025.
Amefafanua kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilianzisha utaratibu wa kliniki hizo pamoja na kamati za ushauri wa kisheria ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, hasa wale wanaoishi mbali na makao makuu ya ofisi hiyo yaliyopo Dodoma.
“Kwa kutambua changamoto ya umbali kwa wananchi, tulianzisha kamati hizi ili malalamiko yaweze kushughulikiwa katika maeneo yao. Wakati wa uzinduzi wa kamati hizi, pia hufanyika kliniki za sheria kwa muda wa wiki nzima,”ameeleza.
Mhe. Johari amesema kuwa,shauri la Bw. Manyako lilikuwa miongoni mwa kesi za kwanza kushughulikiwa, ambapo alilichukua binafsi baada ya kupokea malalamiko yake kuhusu magari hayo matano yaliyodaiwa kushikiliwa isivyo halali.
“Baada ya kusikiliza maelezo yake, niliguswa sana. Jukumu langu ni kuhakikisha haki inatendeka na wananchi wanarejeshewa imani na mfumo wa sheria,”amesema.
Kwa mujibu wa maelezo ya tukio hilo, magari hayo yalichukuliwa na dalali wa mahakama kufuatia mgogoro uliotokana na ajali ya moto katika karakana ya kampuni hiyo.
Hata hivyo, licha ya kampuni kulipa fidia ya uharibifu uliotokea, magari hayo yaliendelea kushikiliwa hadi hatua ya kuingiliwa kati na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Johari amesisitiza kuwa,ofisi yake itaendelea kutumia mbinu za utatuzi wa migogoro nje ya mahakama ili kupunguza mzigo wa mashauri mahakamani na kuongeza ufanisi wa utoaji haki.
“Tunataka wananchi wawe na imani na taasisi za haki. Tutazidi kuboresha huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa ipasavyo,” ameongeza.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga amesema,tukio hilo linaakisi uwajibikaji wa vyombo vya sheria na kuhimiza wananchi kuendelea kuviamini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw. Godwin Gondwe amebainisha umuhimu wa wataalamu wa sheria katika kusaidia viongozi kufanya maamuzi sahihi, akieleza kuwa wanasheria hutoa mwongozo muhimu wa kisheria na kusaidia kubainisha mipaka ya majukumu ya kiutendaji.
Aidha, Gondwe ameeleza kuwa,katika Wilaya ya Singida, zaidi ya wananchi 2,000 wamenufaika na huduma za msaada wa kisheria kupitia kliniki hizo, ambapo mashauri mbalimbali yamefanikiwa kutatuliwa kwa njia mbadala.
Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Neema Ringo amesema, mafanikio ya kurejeshwa kwa magari hayo yanaendana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watendaji wa serikali wanatatua changamoto za wananchi na kurejesha tabasamu kwao.
Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Bw. Manyako amezishukuru taasisi zote zilizohusika katika kufanikisha urejeshwaji huo, akieleza kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa ushirikiano mzuri ndani ya mfumo wa utoaji haki.
“Magari haya yalikuwa na thamani ya takribani shilingi milioni 120. Kurejeshwa kwake kutaiwezesha kampuni kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Singida,”amesema.
Magari yaliyokabidhiwa ni pamoja na Toyota Land Cruiser, Isuzu Winch Truck, Isuzu Tipper Hard Top, Land Rover 101 Station Wagon pamoja na Toyota Land Cruiser Station Wagon.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Mkoa wa Singida, Bi. Matrida Meckson amesema,juhudi za utoaji elimu ya sheria kupitia kliniki hizo zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na namna ya kuzidai.
Kwa ujumla, tukio hilo limeelezwa kuwa, sehemu ya mafanikio ya mkakati wa serikali wa kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani na kuimarisha utawala wa sheria nchini.
Kliniki za sheria bila malipo ni huduma inayotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kutoa ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi, hususan wasio na uwezo, pamoja na kutoa elimu ya sheria ili kuimarisha uelewa wa masuala ya kisheria katika jamii.
Tags
Habari
Kliniki za Kisheria
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Sema Limited
