KIGOMA- Katika Mahakama ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma limefungua shauri la uhujumu uchumi dhidi ya watu wawili wanaodaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za Shule ya Msingi Kiyobera, tukio linalodaiwa kutokea Januari, mwaka 2025.
Shauri hilo, lenye namba ECC. 8474/2026, lilisikilizwa Aprili 21, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Mheshimiwa A. J. Kyamba, huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Abdulrahim Omari.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Abubakari Salumu Choyo (32), mwalimu wa Shule ya Msingi Kiyobera pamoja na Mohamedi Miraji Ramadhani (35), aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na makosa ya rushwa kinyume na vifungu vya 22 na 28(1) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2023.
Makosa hayo pia yanasomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200, marejeo ya mwaka 2023.
Aidha, washtakiwa wanadaiwa kukabiliwa na kosa la kughushi nyaraka kinyume na vifungu vya 333, 335(d)(i) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa, mnamo Januari 11, 2025, mshtakiwa wa kwanza, Bw. Choyo, aliandaa dokezo la kuomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 334,000 kutoka katika akaunti ya shule hiyo, akidai fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya malipo ya wapishi, mwalimu wa kujitolea na gharama za sukari kwa ajili ya chai ya walimu.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa wakati wa kuandaa dokezo hilo, mshtakiwa huyo alikuwa akifahamu kuwa tangu Bw. Ramadhani alipokuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, hapakuwahi kuwepo wapishi waliotajwa kwa majina ya Stella Kipawa na Aneth Jumanne, wala madai ya malipo yaliyodaiwa kufanywa kwa Bi.Hawa Kigiri hayakuwa halali.
Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili, Bw. Ramadhani, anadaiwa kuandaa nyaraka za uongo ikiwemo mkataba wa kazi unaoonesha kuwa alipokea na kulipa kiasi cha shilingi 160,000 kwa wapishi hao, huku akijua kuwa watu hao hawakuwepo.
Aidha, anadaiwa kupitisha dokezo hilo la malipo licha ya kufahamu kuwa halikuwa na uhalisia.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, mshtakiwa wa kwanza alikiri kosa la kwanza linalomkabili, huku mshtakiwa wa pili akikana makosa yote.
Mahakama iliwapa dhamana washtakiwa wote baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa. Shauri hilo limeahirishwa hadi Aprili 27, 2026, litakapotajwa tena kwa ajili ya hatua za awali za usikilizwaji wa kesi (PH).
