NA DIRAMAKINI
JESHI Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika katika matukio mawili tofauti ya vurugu yaliyosababishwa na madai ya kupotea kwa nyeti, hali iliyozua taharuki kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi,ACP Almachius Mchunguzi,tukio la kwanza lilitokea Aprili 5, 2026 majira ya saa 2:00 usiku katika Bar ya Kivuga Point, Kijiji cha Mazingara, Wilaya ya Handeni.
Katika tukio hilo, Santiel John alishambuliwa na kujeruhiwa na watu wawili waliotajwa kuwa ni Vado Mchungu na Fadhili Nuru.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni madai ya Fadhili Nuru kwamba amepoteza nyeti zake na kumtuhumu Santiel John kuhusika. Hata hivyo, uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli na mhusika alikutwa akiwa salama.
Majeruhi alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, huku watuhumiwa wakishikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika tukio la pili lililotokea Aprili 6, 2026 majira ya saa 12:30 jioni katika eneo la Mabanda ya Papa, Jiji la Tanga, watu watatu walikamatwa wakiwa ndani ya gari la abiria aina ya Hiace baada ya kuzua taharuki kwa kumtuhumu abiria mwenzao kwa madai kama hayo ya kupotea kwa nyeti.
Watuhumiwa hao ni Haji Mbwana, Mbwana Mluku na Amiri Rashid. Polisi waliwapeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa uchunguzi wa kitabibu ili kuthibitisha madai yao.
Jeshi la Polisi limeonya wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo zinazoweza kusababisha taharuki na uvunjifu wa amani, na kusisitiza umuhimu wa kufuata sheria badala ya kujichukulia hatua mkononi.
