NA DIRAMAKINI
NCHI ya Lebanon imejiunga rasmi na mataifa kadhaa ya Mashariki ya Kati na Ghuba ikiwemo Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Bahrain, Qatar, Iraq, Kuwait, Jordan, Misri na Oman katika juhudi za pamoja za kuhakikisha usalama wa wasafiri waliokwama kufuatia taharuki ya kiusalama inayoendelea katika ukanda huo.
Hatua hiyo inafuatia tangazo jipya la tahadhari ya usafiri lililotolewa na Serikali ya Marekani, likiwataka raia wake walioko katika nchi zaidi ya 10 za Mashariki ya Kati kuondoka haraka iwezekanavyo kutokana na kuongezeka kwa hatari za kiusalama.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa tahadhari kali inayojulikana kama “DEPART NOW”, ikiwaelekeza raia wake walioko katika mataifa mbalimbali ya ukanda huo kuondoka mara moja.
Tahadhari hiyo imechochewa na kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi na kisiasa, hususan baada ya matukio ya mashambulizi na hatua za kulipiza kisasi kati ya mataifa hasimu.
Ripoti kupitia mashirika ya habari za Kimataifa zinaonesha kuwa, hali hiyo imesababisha kufungwa au kuathiriwa kwa anga katika baadhi ya maeneo, jambo lililopelekea kusitishwa kwa safari nyingi za ndege na hivyo kuwaacha maelfu ya wasafiri wakiwa wamekwama katika viwanja vya ndege, hoteli na maeneo mbalimbali ya transit.
Katika kukabiliana na hali hiyo, nchi mbalimbali zimeanzisha ushirikiano wa dharura kwa lengo la kuweka njia salama za kuwawezesha raia wa kigeni kuondoka katika maeneo hatarishi.
Nchi hizo zinashirikiana na mamlaka za Marekani kuweka vituo maalum vya kuondokea (evacuation points) ikiwemo viwanja vya ndege na mipaka ya nchi kavu.
Lebanon, pamoja na nchi nyingine zilizotajwa, imechukua hatua za ziada kuhakikisha ulinzi na uratibu wa haraka wa usafiri kwa wale wanaotaka kuondoka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kikanda.
Pamoja na jitihada hizo, changamoto bado zinaendelea kuripotiwa, ikiwa ni pamoja na uhaba wa safari za ndege, kufungwa kwa baadhi ya balozi na ubalozi mdogo, pamoja na hatari za kiusalama katika baadhi ya maeneo yenye migogoro mikali.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za kimataifa, mamia ya maelfu ya raia wa kigeni, wakiwemo Wamarekani, wanaaminika kuwa bado wapo ndani ya ukanda huo, huku wengine wakilazimika kusubiri msaada wa serikali zao au kutumia njia mbadala za kuondoka.
Serikali ya Marekani imeendelea kusisitiza umuhimu wa raia wake kufuata maelekezo ya balozi na ofisi za kibalozi, pamoja na kujisajili katika mifumo ya taarifa za dharura ili kupata taarifa sahihi kwa wakati.
Aidha, imewataka wasafiri kutumia njia zote zinazopatikana, ikiwemo usafiri wa kibiashara pale inapowezekana, huku ikiendelea kushirikiana na mataifa mwenyeji kuwezesha safari maalum za kuwaondoa waliokwama.
Hali ya usalama katika Mashariki ya Kati inaendelea kubadilika kwa kasi, na kufanya ushirikiano wa kimataifa kuwa nguzo muhimu katika kulinda maisha ya raia wa kigeni.
Aidha,ushiriki wa Lebanon na mataifa mengine katika juhudi hizi unaonesha umuhimu wa mshikamano wa kikanda katika nyakati za migogoro. (NA).
