Wewe ungefanyaje ukikuta jirani yako anafuga nyoka? Ulanga yamewakutana

NA DIRAMAKINI

MKAGUZI wa Kata ya Milola, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/INSP) Aloyce Andrew, kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo, wamefanikiwa kumuua nyoka aliyekuwa akifugwa na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo la Mavimba, hususan katika njia panda ya mnadani.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, uwepo wa nyoka huyo ulizua hofu miongoni mwa wananchi, hali iliyosababisha baadhi yao kushindwa kuendelea na shughuli za kila siku za kiuchumi kutokana na wasiwasi wa usalama wao.

Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia malalamiko ya wananchi waliomuarifu mkaguzi huyo kuhusu uwepo wa mwananchi anayedaiwa kufuga nyoka huyo bila kufahamika madhumuni yake.

Taarifa hizo zilibainisha kuwa,kitendo hicho kilizua taharuki na sintofahamu katika jamii, huku baadhi ya wakazi wakihofia usalama wao na mali zao.

Akizungumza baada ya tukio hilo, A/INSP Aloyce Andrew aliwataka wananchi kuepuka kujihusisha na imani potofu ambazo mara nyingi huchangia kuvuruga amani na utulivu wa jamii.

Alisisitiza kuwa,vitendo vya aina hiyo havikubaliki na vinaweza kuchochea hofu isiyo ya lazima miongoni mwa wananchi.

Aidha, alimwonya mhusika anayedaiwa kufuga nyoka huyo kuacha mara moja vitendo vinavyosababisha taharuki kwa jamii, akibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na matendo yanayokiuka sheria na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Mkaguzi huyo aliongeza kuwa,imani potofu ni kikwazo kwa maendeleo ya jamii, akieleza kuwa tukio hilo ni mfano hai wa jinsi vitendo hivyo vinavyoweza kuathiri shughuli za kiuchumi na ustawi wa wananchi.

Vilevile, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu vitendo vya uhalifu au viashiria vyake, ili kuwezesha mamlaka husika kuchukua hatua stahiki mapema na kudumisha amani na usalama katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here