PWANI-Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salim Morcase tarehe 07 Aprili, 2026 amekemea vikali tabia ya madereva wa magari yanayosafirishwa kwenda nchi jirani (IT) kupakia abiria kwenye magari hayo kwani ni kinyume na sheria.
Akizungumza madereva hao Aprili 07, 2026 katika kituo cha Polisi Chalinze Kamanda Morcase ameeleza kuwa, magari hayo hayana usajili na hayaruhusiwi kupakia abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine hivyo hatakua na muhali kuchukua hatua kwa dereva yeyote wa IT atakayekamatwa amepakia abiria.
Aidha, amewataka madereva hao kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kujali usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani litaendelea kufanya doria na ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti vitendo hivyo, na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kukiuka sheria.
