NA DIRAMAKINI
KIJANA Rashid Shemndorwa ameanza ukurasa mpya wa maisha akibeba matumaini mapya, ujuzi wa kujitegemea na mtazamo chanya kuhusu mustakabali wake baada ya kifungo cha miaka 15 gerezani ambapo amekabihiwa vifaa vya ujenzi kutoka Jeshi la Magereza Tanzania.
Tukio hilo limejiri Aprili 2, 2026 mkoani Njombe ambapo Jeshi la Magereza Tanzania limemkabidhi vifaa vya ujenzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya uongozi wa juu wa jeshi hilo, kufuatia juhudi zake za kujifunza, kubadilika kitabia na kujiendeleza alipokuwa akitumikia kifungo chake.
Shemndorwa ni miongoni mwa wafungwa waliopata fursa ya mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Magereza Ruanda, kilichopo mkoani Mbeya.
Kupitia mafunzo hayo, amepata ujuzi wa vitendo unaolenga kumwezesha kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii baada ya kuachiliwa kwake.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Njombe, Joseph Mkude alieleza kuwa,hatua hiyo inalenga kuhakikisha wafungwa wanaomaliza vifungo vyao wanarejea katika jamii wakiwa na stadi muhimu za maisha pamoja na uwezo wa kujipatia kipato halali.
Alisisitiza kuwa, juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa jeshi hilo wa kuimarisha mageuzi ya tabia na kupunguza uwezekano wa wahusika kurejea kwenye vitendo vya uhalifu.Kwa upande wake, Shemndorwa alieleza kuwa, mafanikio hayo yametokana na nidhamu, kujituma na dhamira ya dhati ya kubadilika aliyokuwa nayo akiwa gerezani.
Alibainisha kuwa, ujuzi alioupata utakuwa chachu ya kuanzisha maisha mapya yenye tija, huku akiepuka kabisa kurejea kwenye mienendo iliyomfikisha gerezani hapo awali.Aidha, alifafanua kuwa ana mpango wa kurejea mkoani Tanga ili kuanza shughuli za ujenzi kwa kutumia ujuzi alioupata, akiahidi kuwa raia mwema, mwenye kuzingatia sheria na kuwa mfano bora kwa jamii, hususan kwa vijana wengine wanaokabiliwa na changamoto za kimaisha.


