NAIROBI-Mkutano wa 13 wa Pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Amani na Usalama na Baraza la Kisekta la Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umehitimishwa leo jijini Nairobi, Kenya na kuweka bayana vipaumbele vya Jumuiya katika Mabaraza hayo.
Ushirikishwaji wa Wanawake katika masuala ya amani, ulinzi na usalama ni kati ya ajenda zilizojadiliwa na kufanyiwa maamuzi ambapo Jumuiya imepitisha Mpango Mkakati wa kwenda sambamba na wanawake katika ulingo huo. Ajenda hiyo pia ni Utekelezaji wa Azimio la Baraza la Usalama la 1325 (UNSCR 1325) la Umoja wa Mataifa.
EAC pia imejadili kuanzishwa kwa mfumo jumuishi wa tahadhari za mapema katika masuala ya ulinzi, usalama na majanga (EAC Early Warning System).
Aidha, katika kuhakikisha Mfumo wa Jumuiya wa uzuiaji na utatuzi wa migogoro unakuwa na tija, mkutano huu umepitisha Mpango Mkakati wa Ushirishwaji wa Asasi zisizo za kiserikali ili kutekeleza msingi wa ujumuishwaji wa wananchi katika shughuli za kikanda.
Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti, Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Rebecca Kadaga kutoka Jamhuri ya Uganda umesisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa uamuzi na maelekezo yanayotolewa na Mabaraza hayo na kuratibu vyema sera za mambo ya nje ili kukabiliana na changamoto zinazoibuka za usalama na mabadiliko ya kisiasa duniani.
Ajenda zilizojadiliwa zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 huku Tanzania ikiwa tayari imeanza utekelezaji wa ndani wa ajenda hizo ikiwemo kuwa na viongozi mahiri na shupavu wanawake katika sekta za ulinzi na usalama.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobass Katambi (Mb), akiambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Dkt. Faraji Mnyepe, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi.










