Mkusanya mapato Bumbuli mahakamani kwa tuhuma za rushwa na uhujumu uchumi

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Lushoto imemfikisha mahakamani Mkusanya Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli mkoani Tanga, Bw. Haji Issa Mdoe akikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi katika kesi namba 6647/2026.
Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Rose Ngoka, ambapo anashtakiwa kwa makosa mawili ya wizi akiwa mtumishi wa umma, kinyume na vifungu vya 258(1), 265 na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Aidha, anakabiliwa na shtaka la kuisababishia serikali hasara, kinyume na aya ya 10(1) na (4) ya Jedwali la Kwanza, zikisomwa pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200, marejeo ya mwaka 2022.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bw. John Chihangala, alidai kuwa kati ya tarehe 21 Mei 2020 na 16 Novemba 2021, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani Tanga, mshtakiwa akiwa katika wadhifa wake wa Mkusanya Mapato, alitenda kosa la wizi wa fedha kiasi cha shilingi 1,584,600 mali ya halmashauri hiyo.

Ilidaiwa kuwa,mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi na huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria, hali iliyosababisha hasara kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka yote yanayomkabili na kwa sasa yupo nje kwa dhamana, huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here