MSD Kanda ya Dodoma yang’ara katika mageuzi ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba

NA GODFREY NNKO

BOHARI ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma imeendelea kujidhihirisha kuwa mhimili muhimu katika kuimarisha sekta ya afya katika kanda hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati katika vituo vya kutolea huduma.
Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa ameyasema hayo leo Aprili 24,2026 wakati wa semina kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyofanyika katika ofisi za MSD Kanda ya Kati zilizopo Kizota jijini Dodoma.

Amesema kuwa,kanda hiyo kwa sasa inahudumia jumla ya vituo zaidi ya 840 vilivyopo katika mikoa ya Dodoma na Singida, pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.

Huduma hizo zinajumuisha halmashauri 18, zikiwemo nane za Mkoa wa Dodoma, saba za Mkoa wa Singida na moja ya Kiteto.

Amesema, lengo kuu la MSD ni kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati katika vituo vya afya, hatua inayochangia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa mfumo mzima wa huduma za tiba nchini.

Kwa mujibu wa Bi.Jumaa, MSD Kanda ya Dodoma imeweka utaratibu maalum wa ugawaji wa huduma kwa wateja wake, kwa kuwagawa katika makundi mawili.

Kundi la kwanza linajumuisha Mkoa wa Singida, huku kundi la pili likijumuisha Mkoa wa Dodoma pamoja na Halmashauri ya Kiteto.

Amefafanua kuwa, utoaji wa huduma hufanyika kwa mzunguko wa kila baada ya miezi miwili, ambapo kila kundi hupatiwa huduma kwa awamu tofauti.

Utaratibu huo unawezesha kila kundi kuhudumiwa mara sita kwa mwaka, hivyo kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba katika maeneo husika.

“Kwa mfano, iwapo mwezi Aprili tunahudumia Mkoa wa Dodoma, basi mwezi Mei tunahudumia Mkoa wa Singida. Mfumo huu umetusaidia kufikia vituo vyote kwa ufanisi na kwa wakati,” ameeleza Bi.Jumaa

Aidha, Meneja huyo amesisitiza kuwa MSD iko tayari kukabiliana na hali za dharura wakati wowote, hususan pale kunapotokea milipuko ya magonjwa au mahitaji ya ghafla ya vifaa tiba.
Amesema,kuanzia ngazi ya menejimenti hadi watendaji wa chini, taasisi hiyo hushirikiana kwa karibu kuhakikisha usambazaji wa bidhaa unafanyika haraka na kwa ufanisi.

Pia,ameongeza kuwa katika matukio ya dharura, MSD hufanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, ambayo hutoa maelekezo ya haraka kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kutokana na uratibu huo, bidhaa muhimu huweza kusafirishwa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji hadi katika maeneo yaliyoathirika, bila kuchelewa.

Aidha,hatua hizi zinaakisi dhamira ya MSD ya kuokoa maisha na kuimarisha huduma za afya nchini, huku ikiendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa sera za afya kwa manufaa ya wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here