NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw.Mavere Tukai amesema kuwa,sekta ya afya ni mhimili mkuu wa usalama wa taifa, akisisitiza kuwa ustawi wa afya ya jamii una uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Bw.Tukai ameyasema hayo Aprili 24,2026 katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Ofisi za MSD Kanda ya Kati eneo la Kizota jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa,jamii isiyo na afya njema haiwezi kuwa salama wala kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
“Afya ni usalama wa taifa. Jamii ikiwa haina afya haiwezi kuwa salama, na bila usalama hakuna uzalishaji, hivyo hakuna uchumi,” amesema.
Amefafanua kuwa,sekta ya afya inaweza kufananishwa na stuli ya miguu mitatu inayojumuisha fedha, huduma na bidhaa, huku MSD ikiwa na jukumu la kusimamia upatikanaji wa bidhaa za afya.
Alionya kuwa, endapo mguu mmoja kati ya hiyo utayumba, sekta nzima itakuwa katika hatari ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Bw. Tukai amesisitiza kuwa, MSD ina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora, salama, zenye gharama nafuu na zinazowafikia wananchi kwa wakati. Amebainisha kuwa, taasisi hiyo ni kiungo muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa kamilifu nchini.
“Tunasimamia upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya. Bila bidhaa hizo, sekta ya afya haiwezi kuwa kamili.Tunahakikisha bidhaa zote ni bora, salama na zinapatikana kwa wakati,” ameeleza.
Aidha, ametaja majukumu makuu ya MSD kuwa ni pamoja na uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya. Ameongeza kuwa, MSD inasambaza wastani wa asilimia 81 hadi 83 ya bidhaa za afya katika vituo vya umma, huku kiasi kilichosalia kikitolewa na wadau wengine katika ngazi za mikoa.
Katika hatua nyingine, Bw. Tukai amesema kuwa, MSD imepiga hatua kubwa katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo kiwango cha utimilifu kimeongezeka kutoka asilimia 40 katika kipindi cha miaka minne iliyopita hadi zaidi ya asilimia 80 kwa sasa.
Pia,kwa upande wa ushirikiano na vyombo vya habari,Bw.Tukae ameahidi kuwa, MSD itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa waandishi wa habari ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma kuhusu shughuli za taasisi hiyo.
Serikali inasemaje?
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Afya, Mfamasia Bi. Anneth Wilbroad amesema, wizara hiyo inathamini mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii na kuimarisha mawasiliano kati ya sekta ya afya na wananchi.
Naye mwakilishi wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Bi. Magreth Makilika ameipongeza MSD kwa kuendeleza ushirikiano na vyombo vya habari, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano bora wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma.
Kwa upande mwingine, mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa niaba ya Mkurugenzi, Dkt.Rashid Mfaume,Bw. Hassan ameeleza kuwa, wanahabari wana jukumu muhimu katika kuunganisha jamii na taasisi za serikali pamoja na kuelimisha umma kuhusu masuala ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa, vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuchochea maendeleo ya jamii kwa kutoa taarifa sahihi, kuibua changamoto na kusaidia katika utoaji wa suluhisho kupitia mijadala ya umma.
Wahariri
Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mhariri Mkuu wa Gazeti la Habari Leo, Bw. Mgaya Kingoba ameipongeza MSD kwa kuandaa semina hiyo, akisema kuwa imechangia kuongeza uelewa sahihi kuhusu sekta ya afya na kupunguza upotoshaji wa taarifa.
Pia,amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa sahihi na zenye kuaminika kwa wananchi, hasa kuhusu mafanikio ya uwekezaji wa serikali kupitia Wizara ya Afya na MSD.
“Nafasi yetu ni kuwa daraja kati ya serikali na wananchi kwa kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia walengwa. Hili linahitaji weledi na uwajibikaji wa hali ya juu,” amesema.
Kwa ujumla, washiriki wa semina hiyo wamekubaliana kuwa ushirikiano kati Bohari ya Dawa (MSD) na vyombo vya habari ni nyenzo muhimu katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi bora kuhusu afya zao.