EZULWINI-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb.), amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya Utawala wa Mfalme Mswati III zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo uliopo Ezulwini, Eswatini.
Katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na hafla ya kusherehekea miaka 58 ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mfalme Mswati III, yameelezwa mafanikio ya utawala wake pamoja na mshikamano wa kitaifa wa wananchi wa Eswatini.
Mfalme Mswati III, katika hotuba yake ameeleza namna nchi hiyo ilivyopiga hatua za kimaendeleo hususan katika sekta ya miundombinu, afya, viwanda, teknolojia na kukuza kiwango cha elimu kwa wananchi wa Eswatini.
Aidha, Mfalme Mswati III amesisitiza umoja na mshikamano kwa nchi za kikanda na Afrika kwa ujumla.
Sherehe hizo zimehusisha matukio mbalimbali ikiwemo gwaride maalum kwa ajili ya maadhimisho hayo, burudani mbalimbali kama ngoma za asili na maonesho ya heshima kwa kiongozi huyo.
Ziara hiyo nchini Eswatini ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua fursa mpya za ushirikiano kati ya Tanzania na Falme ya Eswatini.














