Polisi watoa onyo kali wanaozusha kupotea viungo vya siri

NA DIRAMAKINI

KATIKA kipindi ambacho dunia inaongozwa na ushahidi wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia, wimbi la uzushi unaodai kupotea kwa viungo vya siri limeibuka na kusababisha taharuki kubwa, vifo na majeruhi katika baadhi ya maeneo nchini, hali inayolazimu Jeshi la Polisi kutoa onyo kali kwa umma.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP David Misime kupitia taarifa aliyoitoa leo ameeleza kuwa, kuenea kwa taarifa hizo zisizo na uthibitisho kumechochea vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia watu wanaodhaniwa kuhusika na matukio hayo.

Amesema kuwa, matukio hayo yameanza kushika kasi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Tunduma, ambapo Aprili 1, 2026 watu watano walifariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia mashambulizi yaliyotokana na imani hizo potofu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali kama hiyo ilijirudia katika Jiji la Mbeya katika maeneo ya Makongolosi na Maendeleo, ambapo watu wawili walijeruhiwa vibaya na kulazwa hospitalini wakipatiwa matibabu.

Aidha, Jeshi la Polisi limekumbusha tukio la awali lililotokea katika eneo la Kimara Mwisho na Mbezi Shule jijini Dar es Salaam mnamo Aprili 3, 2024, ambapo wananchi waliwashambulia watu waliodaiwa kuhusika na vitendo hivyo bila ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Katika tukio la hivi karibuni la Aprili 4, 2026 katika maeneo ya Kabwe na Double J Kalumbulu, jijini Mbeya, watu wawili walijeruhiwa vibaya na mmoja wao kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini, kufuatia tuhuma hizo hizo za uzushi.

Akifafanua zaidi, DCP Misime amesema, uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa madai ya kupotea kwa viungo vya siri hayana ukweli wowote, kwani wahusika wote waliodai kuathirika walikutwa na viungo vyao vikiwa katika hali ya kawaida.

Amesisitiza kuwa,vitendo hivyo vinachochewa na imani za kishirikina zisizo na msingi wa kisayansi, na kuonya kuwa vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi iwapo havitadhibitiwa mapema.

“Wananchi wanapaswa kuacha kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho na badala yake kuamini vyombo vya dola na mifumo rasmi ya uchunguzi,” amesema.

Jeshi la Polisi limesema kuwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na kusambaza uzushi huo au kushiriki katika vitendo vya vurugu vinavyohatarisha maisha ya watu.

Aidha, limewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa sahihi ili kudumisha amani na utulivu wa nchi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha taarifa hizo na watu wanaozisambaza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here