Rais Dkt.Mwinyi afanya uteuzi PBZ na Shirika la Bandari Zanzibar

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameteua viongozi wapya katika taasisi muhimu za kiuchumi, hatua inayolenga kuimarisha utendaji, uwajibikaji na maendeleo ya sekta za fedha na miundombinu visiwani humo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kaimu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,Saleh Juma Mussa uteuzi huo unahusisha nafasi za juu za uongozi katika Benki ya Watu wa Zanzibar na Shirika la Bandari Zanzibar, taasisi ambazo ni mhimili wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Katika uteuzi huo, Juma Hassan Juma Reli ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Kabla ya uteuzi huo, Juma alikuwa mtumishi wa umma aliyestaafu, akiwa na uzoefu mpana katika masuala ya utawala na usimamizi wa taasisi za serikali.

Aidha, Ali Aboud Mzee ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar.

Ali anatajwa kuwa mshauri mkuu wa masuala ya biashara na uchumi kutoka sekta binafsi, jambo linalotarajiwa kuleta mchango chanya katika kuimarisha ushindani na ufanisi wa huduma za bandari.

Uteuzi huu unaanza rasmi Aprili 13, 2026 na unatazamwa kama sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha taasisi zake kwa kuwateua viongozi wenye uzoefu na weledi, sambamba na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Pia,wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaona hatua hiyo kuwa na umuhimu mkubwa katika kuongeza ufanisi wa taasisi za kifedha na miundombinu, hususan katika kipindi ambacho Zanzibar inaendelea kujikita katika kukuza uchumi wa buluu na biashara ya kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here