Watumishi NHIF waiomba Serikali kuruhusu usajili Kifurushi cha Faraja

MANYARA-Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wameiomba Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko huo kuiomba Serikali kuruhusu usajili wa wananchi kupitia kifurushi cha Faraja kinachoiwezesha kaya ya watu sita kunufaika na huduma za bima ya afya kwa gharama nafuu.
Ombi hilo limetolewa jana Aprili 13, 2026 na Watumishi wa NHIF Mkoa wa Manyara mbele ya Bodi ambayo iko katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa shughuli za Mfuko katika mikoa ua Singida, Manyara, Arusha. Kilimanjaro na Tanga.

Akiwasilisha ombi hilo. Meneja wa Mkoa Bw. Emmanuel Mwikwabe alisema kuwa wananchi wameonesha utayari na uhitaji mkubwa wa kujiunga na bima ya afya wakati zoezi la usajili wa kaya zisizo na uwezo likiendelea.
“Mwenyekiti wa Bodi tumeona mwitikio na uhitaji mkubwa wa wananchi kutaka kujiunga na kifurushi cha faraja cha shilingi 150,000/- wakati tulipokuwa kwenye zoezi la kusajili wananchi wasio na uwezo, tunaomba sana utusaidie kuiomba Serikali iruhusu kifurushi hiki ili tuanze kuwasajili,” aliomba Bw. Mwikwabe.

Akizungumza na Watumishi hao, Mwenyekiti wa Bodi Bw. Eliud Sanga, alisema yeye na bodi yake wamepokea ombi hilo na watalifanyia kazi ili wananchi waanze kusajiliwa hivyo akasisitiza kwa wakati huu kuendelea kuwafikia wananchi na kuwapa elimu ya umuhimu wa kuwa na bima ua afya.

Katika hatua nyingine, aliwataka Watumishi hao kupiga vita mtu yeyote anayechochea vitendo vya udanganyifu kwenye huduma zake ili kuwezesha kulipa malipo halali na kulinda uhai na ziada inayopatikana.
"Niwaombe sana kupiga vita mtu yeyote yule ambaye ataonekana anafanya au kuchochea vitendo vya udanganyifu, fuatilieni mianya yote na mnapobaini tu chukueni hatua za kudhibiti udanganyifu wowote, kwa kufanya hivi tutaweza kulinda ziada inayopatikana ambayo itasaidia kuboresha huduma kwa wanachama pamoja na maslahi ya Watumishi kwa ujumla wake,” aliagiza Mwenyekiti wa Bodi.

Alisema kuwa kwa sasa Mfuko umeendelea kuimarika ikilinganishwa na ilivyokuwa awali hivyo akawataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa ushawishi wa wananchi katika kujiunga na Bima ya Afya.
“Bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunawafikia wananchi katika maeneo yao, kuwapa elimu na kuwashawishi ili waweze kujiunga na kuwa na uhakika wa matibabu na kwa kufanya hivi tutakuwa tunatimiza ndoto ya Serikali yetu ya wananchi wote kuwa ndani ya Mfumo wa Bima ya Afya,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine alisisitiza Watumishi kuwa na mahusiano mazuri ya kazi baina yao yatakayowasaidia kuwajenga na kusaidiana katika majukumu yao lakini pia kuleta umoja katika kazini na nje ya mazingira ya kazi.Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka aliwapongeza watumishi hao kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii hususan katika kipindi hiki ambacho utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaendelea kwa usajili wa wananchi wanaotoka Kaya zisizo na uwezo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here