NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi wa Serikali kwa kuteua, kuhamisha, na kupangia vituo vipya baadhi ya viongozi waandamizi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utendaji wa Serikali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 2,2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yanahusisha nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Mabalozi na viongozi wa taasisi za umma.
Katika uteuzi huo, Profesa Palamagamba John Aidan Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu. Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kabudi alikuwa akihudumu katika Ofisi ya Rais – Ikulu akisimamia masuala maalum.
Aidha, Mbunge Reuben Nhamanilo Kwagilwa amehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sasa atahudumu kama Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira.
Katika mabadiliko hayo pia, Dkt. Festo John Dugange amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), ambapo atasimamia masuala ya elimu.
Kwa upande wa uwakilishi wa kidiplomasia, Balozi Said Othman Yakub amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, huku Balozi Ali Jabir Mwadini akiteuliwa kuwa Katibu wa Rais.
Vilevile, Rais amewateua Dkt. Eveline Wilbard Munisi na Bi. Angela Kizigha kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, uteuzi wa Dkt. James Andilile Mwainyekule, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), umetenguliwa na atapangiwa majukumu mengine ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi walioteuliwa katika nafasi za Waziri na Naibu Waziri wataapishwa katika tarehe itakayopangwa baadaye.
Aidha, hatua hizi zinaakisi dhamira ya Rais Samia ya kuimarisha utendaji kazi wa Serikali kwa kufanya maboresho ya mara kwa mara katika safu ya uongozi, ili kuhakikisha huduma bora na maendeleo endelevu kwa wananchi.