DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Kassim Msemo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuimarisha usimamizi wa mifumo ya malipo na ulipaji, akieleza kuwa katika mazingira ya sasa ya kifedha ya kidijitali, hakuna benki kuu inayoweza kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa peke yake.
Bi. Msemo ametoa kauli hiyo wakati wa kufunga kikao cha pamoja cha usimamizi wa mifumo ya malipo na ulipaji kwa nchi za Afrika Mashariki kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 30 Machi hadi 2 Aprili,2026.
Ameeleza kuwa,kwa muda wa siku nne, kikao hicho kimewakutanisha wataalamu mbalimbali waliokuwa na lengo la pamoja la kuimarisha uwazi, uthabiti na ufanisi wa mifumo ya malipo na ulipaji.
Amepongeza kiwango cha ushiriki, uwazi wa mijadala pamoja na kubadilishana uzoefu wa vitendo miongoni mwa washiriki, akibainisha kuwa yote hayo yamewajengea uwezo zaidi katika kutekeleza majukumu yao.
“Ujumbe mmoja muhimu umejitokeza katika majadiliano yetu-katika dunia ya sasa ya mifumo ya fedha ya kidijitali inayokua kwa kasi, ushirikiano wa kikanda si hiari, bali ni lazima,”amesema Bi. Msemo
Aidha, amesisitiza kuwa, kuongezeka kwa muingiliano wa mifumo ya malipo kunahitaji mbinu za pamoja, thabiti na za mbele katika usimamizi, hasa katika maeneo ya usimamizi unaozingatia vihatarishi, uzingatiaji wa kanuni za kupambana na utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (AML/CFT/CPF), ufuatiliaji wa miamala na utawala bora.
Akizungumzia ziara ya washiriki katika huduma ya kifedha ya kidijitali ya Mixx by Yas, Bi. Msemo amesema, imewapatia washiriki uelewa wa vitendo kuhusu fursa na changamoto za ubunifu wa teknolojia ya kifedha (fintech), na kusisitiza kuwa usimamizi madhubuti unapaswa kuzingatia si tu sera bali pia uhalisia wa kiutendaji wa taasisi zinazosimamiwa.
Bi. Msemo amehitimisha kwa kueleza kuwa, Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kujenga na kuimarisha miundombinu ya masoko ya fedha, kuboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi, pamoja na kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sekretarieti ya EAC katika kufanikisha malengo ya pamoja.



