NA DIRAMAKINI
RAIS wa Marekani, Donald Trump amezua mjadala mkubwa kimataifa baada ya kumkosoa vikali kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, kufuatia wito wake wa kusitishwa kwa vita na kuhimiza amani duniani.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV. Picha na Mtandao.
Kauli hiyo kali imetolewa kupitia ujumbe wa mitandao ya kijamii, ambapo Trump amemwelezea Papa Leo XIV kuwa “dhaifu katika masuala ya uhalifu” na “mbaya kwa sera za mambo ya nje,” katika hatua isiyo ya kawaida kwa kiongozi wa kisiasa kumshambulia moja kwa moja kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa duniani.
Mvutano huo unatokana na matamshi ya Papa Leo XIV aliyotoa hivi karibuni akilaani vita vinavyoendelea, hasa vinavyohusisha Marekani, Israel na Iran.
Katika ibada maalum ya maombi ya amani iliyofanyika Vatican, Papa huyo alitoa wito kwa viongozi wa dunia kusitisha umwagaji damu na alikosoa kile alichokiita “udanganyifu wa nguvu za kupindukia” unaochochea migogoro ya kivita.
Aidha, Papa Leo XIV amekuwa mkosoaji wa mara kwa mara wa sera kali za uhamiaji za utawala wa Trump pamoja na msimamo wake kuhusu vita dhidi ya Iran, akisisitiza kuwa maamuzi ya kisiasa yanapaswa kuzingatia utu wa binadamu na misingi ya amani.
Majibu ya Trump
Katika kujibu kauli hizo, Trump ameeleza kutoridhishwa kwake na msimamo wa Papa, akidai kuwa hataki kiongozi wa kidini anayekosoa sera za Rais wa Marekani.
Pia amemshutumu Papa huyo kwa kuwa na mwelekeo wa kisiasa unaoegemea upande wa “mrengo wa kushoto,” akisisitiza kuwa msimamo wake unaweza kudhoofisha maslahi ya Marekani katika diplomasia ya kimataifa.
Kauli hizo zimekuja katika kipindi ambacho mvutano wa kisiasa na kijeshi katika Mashariki ya Kati unaendelea kuongezeka, huku juhudi za kidiplomasia zikikabiliwa na changamoto kubwa.
Hatua ya Trump imelaaniwa na baadhi ya viongozi wa dini na wachambuzi wa siasa, wakieleza kuwa ni nadra kwa Rais wa Marekani kumkosoa hadharani Papa kwa namna hiyo.
Wengi wameeleza kuwa,matamshi hayo yanaweza kuongeza mgawanyiko kati ya taasisi za kisiasa na kidini, hasa katika nyakati za migogoro ya kimataifa.
Kwa upande wake, Vatican haijatoa tamko rasmi kuhusiana na kauli hizo, huku Papa Leo XIV akiendelea na ujumbe wake wa kuhimiza amani, mshikamano na mazungumzo badala ya vita.
Mgogoro huu unaonesha wazi tofauti ya mitazamo kati ya uongozi wa kisiasa na kidini kuhusu namna ya kushughulikia migogoro ya kimataifa.
Aidha,wakati Trump akisisitiza nguvu na usalama wa taifa, Papa Leo XIV anaendelea kusisitiza maadili ya kibinadamu, diplomasia na umuhimu wa amani duniani.

