Rais Dkt.Mwinyi awaapisha wakuu wapya wa wilaya

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewaapisha rasmi wakuu wapya wa wilaya aliowateua hivi karibuni,wakitarajiwa kuonesha uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa shughuli za maendeleo katika maeneo yao ya kiutawala.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika leo Aprili 13, 2026 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na ndugu na jamaa wa viongozi walioapishwa.
Uapisho huu unafanyika ikiwa Rais Mwinyi mara kwa mara amekuwa akiwataka viongozi katika ngazi mbalimbali kufanya kazi kwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuhakikisha sera na mipango ya Serikali inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta maendeleo endelevu.

Pia, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kijamii katika maeneo wanayoyasimamia kote Unguja na Pemba.

Walioapishwa katika hafla hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Mhe. Lailah Burhani Ngozi,Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Mhe. Dkt. Said Haji Mrisho,Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Mhe. Ali Abdalla Said Natepe.


Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Riziki Daniel Yussuf na Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Mhe. Zuhura Mgeni Othman.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla; Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla; Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mwinyi Talib Haji; Mufti Mkuu wa Zanzibar, Saleh Omar Kaabi pamoja na Wakuu wa Mikoa na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hafla ya uapisho wa Wakuu wa Wilaya ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha utendaji kazi wa Serikali katika ngazi za chini, ambapo viongozi hao wanatarajiwa kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali ya Awamu ya Nane na wananchi katika kusimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao ya kiutawala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here