Riba ya Benki Kuu (CBR) yabaki asilimia 5.75 kwa robo ya pili 2026

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka 2026.
Hayo yameelezwa leo Aprili 2,2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Mwenyekiti wa MPC ambaye pia ni Gavana wa BoT. Bw.Emmanuel Tutuba.

Dkt.Kayandabila amewaeleza wadau wa sekta ya fedha pamoja na waandishi wa habari kuwa, uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha kamati ambacho kimeketi Aprili 1,2026 ili kufanya tathimini ya mwenendo wa uchumi.

Amesema,uamuzi huu wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) unalenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya lengo la asilimia 3-5, huku riba ya mikopo ya mabenki ikitarajiwa kubaki nafuu nchini.

"Kutokana na tathmini hiyo, Kamati iliamua kiwango cha Riba ya Benki Kuu kubaki asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka 2026.Kiwango hicho kilionekana ni sahihi kwa sasa katika kudhibiti mfumuko wa bei kubakia ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5."

Aidha, amesema kiwango hicho kitawezesha kupunguza athari za mgogoro wa kisiasa unaoendelea Mashariki ya Kati kwenye uchumi wa nchi yetu. "Mgogoro huo umeathiri biashara, uwekezaji, na ustahimilivu wa uchumi wa dunia."

Dkt.Kayandabila amesema, kamati imeamua kupunguza wigo wa riba ya Benki Kuu kutoka asilimia +/-2 hadi asilimia +/-1.5, kuanzia mwezi Aprili 2026. 

Lengo la hatua hii ni kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa sera ya fedha katika kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo na kuchochea ukuaji wa uchumi. 

Kufuatia uamuzi huu, wigo wa riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki utakuwa kati ya asilimia 4.25 hadi asilimia 7.25 kwa robo ya pili ya mwaka 2026. 

Amesema, Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kuwa riba ya mikopo ya siku 7 baina ya benki inabaki ndani ya wigo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here