Sekta ya Fedha yajipanga upya,jukwaa laweka mkazo uchumi usiotumia fedha taslimu nchini

DAR-Kikao cha 13 cha Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2026 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, kimejadili masuala muhimu katika sekta ya fedha na kukubaliana kuharakisha mchakato wa kuijenga Tanzania kuelekea uchumi unaotumia fedha taslimu kwa kiwango kidogo zaidi.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni Mfumo wa Usimamizi wa Majanga wa Sekta ya Fedha, Mfumo wa Usalama wa Kidijitali katika Sekta ya Fedha, pamoja na Ripoti ya Uthabiti wa Sekta ya Fedha 2025.

Katika eneo la mfumo wa usimamizi wa majanga katika sekta ya fedha, jukwaa lilijadili namna bora ya kuimarisha uratibu katika maandalizi, usimamizi na utatuzi wa migogoro, kwa kuzingatia mbinu bora za kimataifa ikiwemo miongozo ya Bodi ya Uthabiti wa Kifedha.

Aidha, jukwaa lilijadili uwezekano wa kuanzishwa kwa mfuko wa ulinzi wa wamiliki wa bima, mfuko wa ulinzi wa wawekezaji, pamoja na mipango ya dhamana ya akiba kwa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOs), ili kusaidia utatuzi kwa gharama ndogo na kuimarisha imani katika sekta ya fedha.
Katika eneo la usalama wa kidijitali, Jukwaa lilipokea na kujadili kuhusu Vithibiti vya kiufundi na kiutendaji vya usalama wa mtandao ikiwemo mifumo ya kinga dhidi ya mashambulizi ya mtandao, usimamizi wa vihatarishi vya kidijitali, ufuatiliaji wa miamala na mifumo, pamoja na hatua za kuimarisha mwendelezo wa huduma za kifedha wakati wa matukio ya dharura.

Jukwaa lilikubaliana kuwa uimarishaji wa hatua hizo ni muhimu katika kulinda uthabiti wa sekta ya fedha sambamba na kuendeleza matumizi salama ya huduma za kifedha za kidijitali, hususan katika safari ya kuelekea uchumi wa matumizi kidogo ya fedha taslimu.

Aidha, Jukwaa lilipendekeza kubuniwa kwa mkakati mahsusi utakaoharakisha kufikiwa kwa lengo hilo nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa mifumo ya malipo, kupunguza gharama za miamala, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Jukwaa hilo linawakutanisha wajumbe 15 kutoka ofisi mbalimbali za serikali pamoja na taasisi zinazosimamia sekta ya fedha, likiwa na lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano katika kulinda uthabiti wa sekta ya fedha nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here