NA DIRAMAKINI
OFISI ya Rais, Maendeleo ya Vijana imetangaza rasmi matokeo ya awamu ya kwanza ya maombi ya mikopo kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, huku ikiwataka waombaji kuzingatia ubora wa maandalizi ya miradi na uwasilishaji sahihi wa nyaraka ili kuongeza uwezekano wa kunufaika na fursa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 28,2026 na kitengo cha mawasiliano cha ofisi hiyo, dirisha la kwanza la maombi lilifunguliwa Machi 21, 2026, likilenga kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mwitikio wa vijana ulikuwa mkubwa, jambo linalodhihirisha uhitaji na ari ya vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Katika hatua ya awali ya uchambuzi wa maombi, orodha ya waombaji wa awamu ya kwanza imewasilishwa katika Benki ya CRDB kwa ajili ya uhakiki.
Baada ya kukamilika kwa mchakato huo, waombaji watakaothibitishwa kuwa na sifa stahiki watapatiwa mafunzo maalum yatakayolenga kuwajengea uwezo wa kusimamia na kutumia mikopo kwa tija.
Mafunzo hayo yatadumu kwa siku tatu na yatahusisha masuala muhimu ikiwemo elimu ya biashara, usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo pamoja na ujuzi wa uendeshaji wa miradi kulingana na sekta husika.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika katika ngazi ya kanda, ambapo ratiba kamili itatangazwa rasmi mwezi Mei, 2026.
Aidha, Serikali imebainisha changamoto zilizojitokeza katika maombi ya awamu ya kwanza, ikiwemo upungufu wa ujuzi katika uandishi wa miradi na kutokamilika kwa nyaraka muhimu kulingana na matakwa ya tangazo.
Kutokana na hali hiyo, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana imeona umuhimu wa kuendesha mafunzo ya ziada kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kuandaa maombi yenye ubora zaidi katika awamu zijazo.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika programu hii endelevu, na kuhakikisha kuwa fursa zinazotolewa zinafikiwa na vijana wengi zaidi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mpango wa utoaji mikopo kwa vijana ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukuza ajira, ubunifu na maendeleo ya uchumi jumuishi, ambapo vijana wanahimizwa kuchangamkia fursa hizo kwa kuzingatia vigezo na miongozo inayotolewa.
Serikali imewahakikishia vijana kuwa itaendelea kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo ili kuhakikisha uwazi, ufanisi na usawa katika upatikanaji wa rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
ORODHA YA WANUFAIKA WA MIKOPO YA VIJANA AWAMU YA KWANZA


