NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, Crescentius Magori amesema, klabu hiyo imejipanga kuwasilisha shauri katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (Court of Arbitration for Sport-CAS) pamoja na kuliandikia Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kufuatia sakata la usajili na uraia wa mchezaji wa Young Africans SC, Mohamed Damaro Camara.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Magori amesema baada ya tathmini ya kina, klabu yake imebaini uwepo wa dosari zinazoweza kuhatarisha misingi ya ushindani wa haki katika ligi.
Ameeleza kuwa, kuna viashiria vinavyoonyesha uwezekano wa baadhi ya klabu kutumia mianya ya kikanuni ili kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kuliko inavyoruhusiwa.
“Tumefanya tathmini ya kina na kubaini kuwa kuna mambo hayajakaa sawa. Inaonekana kuna klabu inanufaika na hali hii kwa kuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa. Hivyo, pamoja na kupeleka suala hili CAS, pia tutaliwasilisha FIFA kwa hatua zaidi,” amesema Magori.
Magori ameongeza kuwa, klabu hiyo ilishawahi kuwasilisha barua mwaka uliopita kuhusu mabadiliko ya uraia wa baadhi ya wachezaji, lakini haikupata majibu hadi sasa. Amesema hali hiyo inazua maswali kuhusu usawa na uwazi katika usimamizi wa ligi.
Aidha, amesisitiza kuwa suala hilo linaibua hoja nzito kuhusu haki na ulinganifu wa ushindani, akidai kuwa kuna uwezekano wa baadhi ya timu kutumia mianya hiyo kujipatia faida isiyo halali.
Hata hivyo, kwa upande wake, Shirikisho la Soka Tanzania (Tanzania Football Federation-TFF) kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, tayari lilishatupilia mbali shauri la Simba lililokuwa likipinga uhalali wa usajili wa mchezaji Mohamed Damaro Camara kuichezea Yanga.
Hatua ya Simba kupeleka suala hilo katika vyombo vya juu vya kimataifa inaashiria kuendelea kwa mvutano wa kisheria ambao unaweza kuwa na athari pana kwa usimamizi wa ligi na kanuni za usajili wa wachezaji nchini.
.jpeg)