Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imetoa taarifa kwa umma ikikanusha uvumi unaosambaa mitandaoni kuhusu uwepo wa kapsuli za dawa zenye vitu vinavyofanana na misumari midogo.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Aprili 6, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adamu Fimbo, amesema kuwa video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii imeandaliwa kwa lengo la kupotosha umma na kuzua hofu isiyo na msingi.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, video hiyo inaonesha mtu akifungua kapsuli na kutoa vitu vya kigeni, jambo ambalo linaelezwa kuwa ni mbinu inayotumiwa na baadhi ya watu wasio waaminifu kutengeneza maudhui ya kushtua.
Aidha, mamlaka hiyo imefafanua kuwa dawa zote zinazoingia nchini hukaguliwa kwa umakini mkubwa, na viwanda vya dawa hutumia mashine za kisasa zinazozalisha maelfu ya vidonge kwa dakika, hivyo haiwezekani kitaalamu kwa msumari kuingizwa ndani ya kapsuli moja moja.
Imeongeza kuwa iwapo kungekuwa na kitu kigumu kama msumari ndani ya kapsuli, mashine za kufunga dawa zingeharibika au kushindwa kufanya kazi ipasavyo, jambo ambalo halijawahi kuripotiwa katika mifumo ya uzalishaji wa dawa.
Kutokana na hali hiyo, TMDA imewashauri wananchi kuendelea kutumia dawa kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya, na kuhakikisha wanazinunua katika sehemu zilizosajiliwa kama famasi, maduka ya dawa muhimu, pamoja na vituo vya afya vinavyotambulika.
Halikadhalika, mamlaka hiyo imewataka wananchi kutoa taarifa rasmi wanapobaini kasoro yoyote kwenye dawa badala ya kusambaza taarifa mitandaoni, na imeonya kuwa kueneza uvumi huo kunaweza kuathiri matibabu ya wagonjwa na kusababisha hofu isiyo na sababu.
