Tanzania yaongeza kasi mageuzi makazi holela

NAIROBI-Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha makazi holela na kuyageuza kuwa maeneo rasmi, salama na yenye huduma bora, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na kasi kubwa ya ukuaji wa miji nchini.
Hayo yameelezwa jijini Nairobi nchini Kenya na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt.Leonard Akwilapo katika mjadala maalum uliofanyika pembezoni mwa Kongamano la Pili la Miji Afrika (2ND Africa Urban Forum), ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili mbinu jumuishi za kuleta mageuzi katika makazi holela.
Amesema, Tanzania kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea, inashuhudia ongezeko kubwa la watu wanaohamia mijini, hali inayosababisha shinikizo katika upangaji wa miji, utoaji wa makazi, usimamizi wa ardhi pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa, katika kipindi cha zaidi ya nusu karne, idadi ya watu wanaoishi mijini imeongezeka kwa kasi kutoka asilimia 5.7 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 34.9 mwaka 2022, huku makadirio yakionesha kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hiyo itafikia asilimia 59.

‘’Ukuaji huu unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kasi ya ukuaji wa miji katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara,’’amesema.

Amesema, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya Watu ya mwaka 2000 pamoja na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 iliyoboreshwa mwaka 2023, zinaelekeza wazi kuwa makazi holela yataboreshwa na kurasimishwa ili kuhakikisha wakazi wanapata haki ya umiliki wa ardhi na huduma za msingi.
Aidha, Dkt.Akwilapo amesema, Serikali ya Tanzania pia imeanzisha programu maalum ya upangaji upya wa ardhi (land readjustment) inayolenga kuboresha maeneo chakavu yaliyopo katikati ya miji, ili kuyafanya yaweze kutumika kwa ufanisi zaidi kiuchumi na kijamii.

Akihitimisha wasilisho lake Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisisitiza kuwa makazi holela hayapaswi kuonekana kama tatizo pekee, bali kama sehemu ya fursa za kiuchumi na ubunifu kwa wananchi wengi.
Alitoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana katika kuunganisha mipango rasmi ya miji na hali halisi ya makazi holela, ili kujenga miji himilivu, jumuishi na inayokidhi mahitaji ya wote bila kumuacha mtu nyuma, kwa kuzingatia malengo ya Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here